Qassemi: Iran haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49990-qassemi_iran_haitasalimu_amri_mbele_ya_mashinikizo_ya_marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Marekani imeanzisha makundi katika maeneo mbalimbali ya dunia hususan katika nchi jirani na Iran kwa shabaha ya kuzuia ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo na Tehran, lakini Jamhuri ya Kiislamu itavuka salama kipindi cha sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 06, 2018 03:59 UTC
  • Bahram Qassemi
    Bahram Qassemi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Marekani imeanzisha makundi katika maeneo mbalimbali ya dunia hususan katika nchi jirani na Iran kwa shabaha ya kuzuia ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo na Tehran, lakini Jamhuri ya Kiislamu itavuka salama kipindi cha sasa.

Bahram Qassemi amesema kuwa, Marekani itajuta kuhusiana na hatua zake hizo dhidi ya Iran na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitakuwa mateka wa mashinikizo ya serikali ya Washington kwa sababu inazo nyenzo nyingi zinazoiwezesha kukabiliana na mashinikizo hayo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria suala la kujiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusema: Nchi nyingi duniani zinaafiki kuendelea kuwepo makubaliano ya nyuklia ya kundi la 5+1 na Iran, kwa sababu hiyo Marekani inajihisi unyonge na udhaifu na imeamua kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran.

Vilevile amezungumzia hali ya eneo la magharibi mwa Asia na kusema kuwa, eneo la Mashariki ya Kati linasumbuliwa na changamoto nyingi na halina utulivu. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, sera za Jamhuri ya Kiislamu ni kupanua zaidi ushirikiano na nchi jirani.