Iran: Nchi za Ulaya si wakweli katika suala la kupambana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i50754-iran_nchi_za_ulaya_si_wakweli_katika_suala_la_kupambana_na_ugaidi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani uamuzi usio na mantiki na wa kushangaza uliochukuliwa na Umoja wa Ulaya wa kuwawekea vikwazo raia kadhaa wa Iran kwa kutegemea tuhuma zisizo na msingi wowote.
(last modified 2026-02-25T11:30:13+00:00 )
Jan 09, 2019 17:00 UTC
  • Iran: Nchi za Ulaya si wakweli katika suala la kupambana na ugaidi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani uamuzi usio na mantiki na wa kushangaza uliochukuliwa na Umoja wa Ulaya wa kuwawekea vikwazo raia kadhaa wa Iran kwa kutegemea tuhuma zisizo na msingi wowote.

Umoja wa Ulaya, ambao unadai kwamba unajitahidi kuhakikisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yanalindwa, jana Jumanne ulianza kutekeleza duru ya kwanza ya vikwazo dhidi ya Iran tangu yalipoanza kutekelezwa makubaliano hayo mwaka 2016; vikwazo ambavyo vimetokana na madai yaliyotolewa na Denmark dhidi ya Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Tehran ni ishara ya kutokuwa wakweli nchi za Ulaya katika suala la kupambana na ugaidi; na akaongezea kwa kusema: Badala ya Umoja wa Ulaya kuyaweka kwenye orodha ya vikwazo vyake makundi ya kigaidi na ya utendaji jinai kama Munafiqina (MKO) na Al-Ahvaziyah, unayaunga mkono makundi hayo.

Kundi la kigaidi la Munafiqina (MKO) linaendesha harakati zake kwa uhuru katika nchi za Ulaya ikiwemo Ufaransa

Bahram Qassemi ameeleza bayana kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mbeba bendera wa mapambano dhidi ya ugaidi katika eneo; na usalama ilionao Ulaya imeupata kutokana na juhudi hizo za Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kwamba: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itajibu mapigo kwa kuchukua hatua zinazofaa mkabala wa hatua hiyo ya EU.

Itakumbukwa kuwa, pasi na kutoa ushahidi wowote, mnamo tarehe 30 Oktoba mwaka uliopita wa 2018, Denmark iliituhumu Iran kwamba inapanga kufanya hujuma ya shambulio ndani ya ardhi ya nchi hiyo, tuhuma ambazo Jamhuri ya Kiislamu ilizikanusha.

Hii ni pamoja na kwamba, Benjamin Netanyahu,Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel alitangaza waziwazi kuwa, Israel imehusika moja kwa moja katika upikaji wa jungu hilo la fitina ya kesi iliyobuniwa na Denmark dhidi ya Iran.../