Iran yazindua nyambizi mpya yenye makombora ya cruise
(last modified Mon, 18 Feb 2019 02:33:36 GMT )
Feb 18, 2019 02:33 UTC
  • Iran yazindua nyambizi mpya yenye makombora ya cruise

Rais Hassan Rouhani wa Iran amezindua nyambizi ya kisasa iliyoundwa hapa nchini ambayo ina uwezo wa kusheheni makombora ya cruise.

Nyambizi hiyo iliyopewa jina la Fateh imezinduliwa katika sherehe iliyofanyika Jumapili katika mji wa bandarini wa Bandar Abbas.

Nyambizi ya Fateh ambayo kwa asilimia 100 imeundwa kwa kutegemea teknolojia iliyobuniwa na wataalamu Wairani inaweza kuenda mita 200 katika kina cha bahari kwa muda wa wiki tano mfululizo.

Nyambizi hii ambayo ni ya kwanza ya aina yake inayomilikiwa na Iran ina uwezo wa kubeba na kufyatua makombora ya cruise ikiwa chini ya maji.

Aidha nyambizi hiyo yenye uzito wa tani 527 ina silaha nyingine za kisasa kama vile torpedo na mabomu ya chini ya maji.

Nyambizi ya Fateh

Hali kadhalika nyambizi ya Fateh ina mfumo erevu wa kuongoza makombora na rada ya kisasa aina ya Sonic ambayo inaweza kutambua haraka manowari za kivita za adui.

Mwezi Novemba mwaka 2018 pia Iran ilizindua nyambizi mbili za daraja la Ghadir ambazo zina uwezo wa kurusha makombora kutoka chini ya bahari.

Katika miaka ya hivi karibuni Iran imeweza kuzindua nyambizi kadhaa za kisasa zilizoundwa humo nchini kama vile Qaem, Nahang, Tareq na Sina.

 

Tags