Katibu Mkuu wa UN ataka India, Pakistan zipunguze uhasama
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa India na Pakistan zichukue hatua za haraka kupunguza uhasama baina yao kufuatia hujuma mbaya ya kigaidi huko Kashmir ambayo imepelekea kuwepo hatari ya kuibuka mapigano baina ya nchi hizo mbili zenye silaha za nyuklia.
Hali ya wasiwasi baina ya nchi hizo mbili jirani na mahasimu wa jadi ilijitokeza baada ya hujuma ya kigaidi katika eneo linalozozaniwa la Kashmir kupelekea askari 40 wa India kuuawa mnamo Februari 14.
India imeilaumu Pakisan kuwa inawapa hifadhi magaidi tuhuma ambazo Pakistan imekanusha. Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stepane Dujarric amesema umoja huo una wasiwasi mkubwa kufuatia kuendelea kutokota uhasama baina ya Pakistan na India. Amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kupatanisha pande mbili hasimu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Shah Mahmood Qureishi tayari ameomba Umoja wa Mataifa upatanishe pande mbili.
Jummane Kamanda Mkuu wa Majeshi ya India K.J.S Dhillon alisema hujuma iliyotekelezwa Kashmir iliratibiwa na Shirika la Kijasusi la Jeshi la Pakistan ISI. Naye Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amesema nchi yake itatoa jibu kali kwa hujuma iliyopelekea askari wa nchi hiyo kuuawa Kashmir. Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan amesema nchi yake haitasita kulipiza kisasi.
Kashmir ni jimbo lenye Waislamu wengi India na limekuwa lilikumbwa na mzozo tokea India na Pakistan zipate uhuru kutoka Uingereza mwaka 1947. Eneo moja la Kashmir liko Pakistan na lingine liko India. Hujuma ya kigaidi iliyoibua mzozo mpya ilijiri katika eneo la Kashmir linalotawaliwa na India.