Iran: Watu wenye ushawishi wakabiliane na hatua zisizo za kibinadamu za Marekani
(last modified Sun, 07 Apr 2019 07:51:52 GMT )
Apr 07, 2019 07:51 UTC
  • Iran: Watu wenye ushawishi wakabiliane na hatua zisizo za kibinadamu za Marekani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezitaka nchi na watu wenye ushawishi duniani kupambana na mienendo na hatua zisizo za kibinadamu za Marekani.

Bahram Qassemi amesema hayo katika mahojiano na mtandao wa habari wa Al-ahd wa Lebanon na kuongeza kuwa, vikwazo vya Marekani dhidia ya Iran vimezuia misaada ya kibinadamu kutoka nje ya nchi kuwafikia waathiriwa wa mafuriko hapa nchini.

Amesema vikwazo hivyo vinaashiria namna Marekani isivyoheshimu haki za kibinadamu.

Ifahamike kuwa, Marekani imefunga akaunti za Shirika la Hilali Nyekundu, hatua ambayo imefunga milango ya kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa waathiriwa wa mafuriko hapa nchini.   

Shughuli za uokoaji katika eneo lililokumbwa na mafuriko Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, Marekani inabeba dhima ya taathira hasi kwa wahanga wa mafuriko, na hii ni katika hali ambayo hata katika vita vikubwa hakuna mtu anayeweza kuzuia ufikishwaji wa misaada ya kibinadamu ya mashirika kama Hilali Nyekundu na Msalaba Mwekundu.

Wakati huohuo, idadi ya watu waliopoteza maisha katika wiki mbili za mafuriko katika maeneo ya kaskazini mwa nchi imeongezeka na kufikia watu 70.