Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi: Udugu wa Jeshi na IRGC ni harakati maridadi baada ya hatua chafu ya Marekani
(last modified Wed, 17 Apr 2019 13:56:16 GMT )
Apr 17, 2019 13:56 UTC
  • Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi: Udugu wa Jeshi na IRGC ni harakati maridadi baada ya hatua chafu ya Marekani

Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote ya Iran amesema umoja unaozidi kuimarika wa majeshi y Iran ni jambo ambalo limemkasirisha adui na kuongeza: "Mkondo wa udugu kati ya Jeshi la Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ni harakati maridadi baada ya harakati chafu ya Marekani."

Ayatullah Khamenei, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran ameyasema hayo Jumatano mjini Tehran wakati aliponana na Makamanda wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema jeshi la Iran lina wacha Mungu na watendaji kazi bora zaidi ya wakati wowote ule. Huku akilipongeza jeshi na vikosi vingine vya ulinzi vya Iran kwa uwepo wao athirifu katika kuwatumia misaada waathirika wa mafuriko, amesema: "Kila kazi ambayo inamkasirisha adui ni nzuri na hivyo wote wanapaswa kujizuia na kitendo chochote ambacho kinampa motisha adui."

Kiongozi Muadhamu amesema lengo la matamshi yasiyo na msingi ya wakuu wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kudhoofisha moyo wa wananchi. Akibainisha zaidi ameongeza kuwa: "Marekani hivi sasa inakumbwa na madeni ya mabilioni ya dola na sasa baada ya kupita muda mrefu tokea kujiri tufani na mafuriko katika maeneo kama vile California, serikali ya Marekani bado haijaweza kutatua matatizo ya wananchi na kuwalipa fidia lakini pamoja na hayo inatoa matamshi kwa lengo la kudhoofisha motisha wa taifa la Iran."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano na makamanda wa Jeshi la Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameashiria uwepo wa jeshi na vikosi vya ulinzi vya Iran katika eneo na namna vinavyokabiliana na fitina za adui na kuhoji kuwa, "Je, iwapo askari katika Jeshi na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu hawangeingia katika medani kupambana na ISIS (Daesh) leo eneo na nchi jirani zingekuwa katika hali gani na ni kina nani wangekuwa wanatawala?

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, kila moja ya nchi husika zilichukua hatua za lazima katika medani hiyo lakini pamoja na hayo majeshi ya Iran yalikuwa na nafasi muhimu isiyoweza kupuuzwa na leo kwa hakika baraka za majeshi ya Iran hazionekani tu nchini Iran bali pia katika nchi zingine.

Amiri Jeshi Mkuu wa Iran aidha ametoa salamu zake za pongezi kwa munasaba wa Siku ya Jeshi na kusema, vikosi vya kijeshi ni dhihirisho la nguvu za kitaifa na kuongeza kuwa: "Katika nchi nyingi hata zile zinazodai kuwa na uhuru na haki za binadamu, vikosi vya kijeshi huwa ni nguvu ya kidikteta na ya kukabiliana na mataifa na nukta hii inaonekana wazi siku hizi katika matukio yanayojiri Paris n.k."

Tags