May 03, 2019 11:27 UTC
  • Ayatullah Khatami: Siri ya taifa la Iran kuishinda Marekani ni umoja na mshikamano

Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, muono wa mbali, kuwa na mahudhurio katika medani, kusimama kidete, umoja na mshimano ndio siri ya ushindi wa taifa la Iran mbele ya Marekani na washirika wake.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema hayo leo mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya kimaanawi na kisiasa ya Swala ya Ijumaa ambapo amebainisha kwamba, katika kipindi chote cha miaka 40 iliyopita hakuna wakati ambao Marekani haikuwa katika chuki na taifa la Iran.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amebainisha kuwa, licha ya njama mtawalia na chuki zisizo na kikomo za Marekani dhidi ya Iran, lakini daima wananchi wa Iran walizishinda njama za Washington na waitifaki wake.

Ayatullah Khatami amekumbusha vitisho vya hivi karibuni vya Marekani dhidi ya Iran na kubainisha kwamba, tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ubeberu wa dunia ukiongozwa na Marekani ulikuwa katika vita vya kijeshi, vya kiuchumi, vya kisiasa na kiuchumi dhidi ya Iran.

Swala ya Ijumaa- Tehran

Aidha amesema taifa la Iran limepata ushindi pia katika vita vya kiuchumi vya hivi karibuni.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya wiki hii hapa mjini Tehran ameashiria siasa za kibabe na za kupenda makuu za serikali ya Marekani na kueleza kwamba, viongozi wa Washington wamesimama dhidi ya mataifa mengine ikiwemo Venezuela  na wanamuunga mkono kibaraka (kiongozi wa upinzani nchini Venezuela) dhidi ya serikali halali na iliyochaguliwa na wananchi ya Rais Nicolas Maduro.

Tags