Rouhani: Iran itatoa jibu mwafaka iwapo anga yake itahujumiwa tena
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54364-rouhani_iran_itatoa_jibu_mwafaka_iwapo_anga_yake_itahujumiwa_tena
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran haifuatilii kuingia vitani na Marekani lakini itatoa jibu mwafaka iwapo anga yake itahujumiwa tena na Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 25, 2019 22:54 UTC
  • Rouhani: Iran itatoa jibu mwafaka iwapo anga yake itahujumiwa tena

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran haifuatilii kuingia vitani na Marekani lakini itatoa jibu mwafaka iwapo anga yake itahujumiwa tena na Marekani.

Rais Rouhani alisema hayo jana Jumanne katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron ambapo ameashiria kuhusu kutunguliwa ndege isiyo na rubani (drone) ya Marekani baada ya kukiuka anga ya Iran.

Dakta Rouhani amesema "Iwapo Wamarekani watathubutu tena kukiuka maji na anga ya Iran, vikosi vya Iran havitasita kutoa jibu mwafaka. Iran haitaki kuburuzwa vitani na Marekani, lakini katu haitaruhusu uvamizi wowote dhidi yake."

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilitangaza alfajiri ya siku ya Alkhamisi iliyopita kwamba, kikosi cha anga cha jeshi hilo kiliitungua ndege isiyo na rubani ya Marekani baada ya kukiuka sheria na kuingia katika anga ya Iran kwenye mkoa wa Hormuzgan katika Ghuba ya Uajemi. 

Marekani haijaweza kutoa ushahidi wowote wa maana kuthibitisha madai yake kuwa eti droni hiyo ilitunguliwa katika anga ya kimataifa. Rais wa Iran amesema Tehran daima imekuwa ikijitolewa kudhamini usalama na uthabiti katika eneo.

Mabaki ya drone ya Marekani iliyotunguliwa na IRGC

Kwengineko katika mazungumzo yake na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Rais Rouhani amegusia hatua ya Marekani ya kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia, ambapo amesisitiza kuwa katu Tehran haiwezi kufanya mazungumzo mapya kuhusu mapatano hayo ya kimataifa yanayofahamika kama JCPOA.

Kwa upande wake, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameeleza kusikitishwa kwake na hatua ya Rais Donald Trump ya kuiondoa Marekani kwenye mapatano hayo mnamo Mei mwaka jana, akisisitiza kuwa Paris inafanya kila iwezalo kuyanurusu mapatano hayo ya kimataifa.