Jul 01, 2019 12:16 UTC
  • Zarif: Iran haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua zinazochukuliwa na Marekani dhidi ya Iran na kusema kuwa, Wairani kamwe hawatasalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo leo Jumatatu katika marasimu ya kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya Viwanda na Madini hapa Tehran na kubainisha kuwa, mashinikizo ya Marekani dhidi ya Iran hayaashirii kuwa na nguvu na uwezo mkubwa taifa hilo la kibeberu wala kuonyesha kuwa taifa hili ni dhaifu.

Amesema Jamhuri ya Kiislamu inafanya kazi na kushirikiana na mataifa mengine ya dunia ili kuipa funzo Marekani juu ya namna ya kuamiliana na kuzungumza kwa lugha ya heshima na isiyo ya vitisho na taifa hili.

Dakta Zarif amesema mwaka uliopita Marekani ilifanya juu chini na kuchukua hatua ya mbali zaidi ya kulirai mara nne Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanya kikao cha kutafuta eti muafaka dhidi ya Iran, lakini ombi lao hilo liligonga mwamba.

Mei 8 mwaka 2018, Rais Trump alichukua uamuzi wa upande mmoja na kuiondoa Marekani katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kwa kusimama kidete na kutotetereshwa na mashinikizo ya maadui, taifa hili limeweza kuimarisha izza na heshima yake katika eneo, katika hali ambayo Marekani imezidi kutengwa na kuchukiwa.

Baada ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA Mei mwaka jana, Marekani ilitangaza kuiwekea Iran vikwazo ikiwa ni pamoja na kuzuia uuzaji wa mafuuta ghafi ya petroli ya Iran nje ya nchi.

 

Tags