Magaidi wawaua shahidi askari 2 wa Iran katika mpaka wa Pakistan
Wanachama wawili wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) wameuawa shahidi katika makabiliiano na magaidi kusini mashariki mwa nchi, karibu na mpaka wa Pakistan.
Kanali ya Press TV ya Iran imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, maafisa usalama waliouawa shahidi katika makabiliano hayo ya leo Jumapili ni wanachama wa kikosi cha Quds cha IRGC.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limetoa mkono wa pole kwa taifa la Iran kutokana na mauaji hayo ya walinzi wa mipaka na kusema kuwa, mashambulizi kama hayo ya kigaidi yanadhihirisha udhaifu wa maadui wa Jamhuri ya Kiislamu.
Mapema mwezi huu, askari wawili wa SEPAH waliuawa shahidi katika hujuma nyingine ya magaidi dhidi ya kambi ya jeshi ya Hamzeh Seyyed al-Shuhada, katika kaunti ya Piranshahr mkoani Azerbaijan Magharibi.
Kadhalika Februari mwaka huu, kituo cha kikosi cha nchi kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) kilitangaza kuwa, askari 27 waliuawa shahidi na wengine 13 kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi lililotokea kwenye mkoa wa Sistan na Baluchestan huko kusini mashariki mwa Iran.
Makundi ya kigaidi yenye itikadi na fikra za kisalafi na Kiwahabi mipakani ni miongoni mwa magenge yanayoshirikiana na makundi ya kitakfiri na kigaidi yanayoungwa mkono na watawala wa Riyadh kutekeleza hujuma dhidi ya maafisa usalama wa Iran hususan katika maeneo ya mipakani.