Dakta Zarif: Nimewekewa vikwazo baada ya kukataa pendekezo la kukutana na Trump
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria safari yake ya mwezi uliopita huko New York na kusema kuwa, "niliambiwa nitawekewa vikwazo katika kipindi cha wiki mbili zijazo isipokuwa kama nitakubali kukutana na Rais Donald Trump wa Marekani."
Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari na kueleza kwamba. licha ya Wamarekani kudai na kupigia debe uhuru wa kutoa maoni, lakini hawana imani na kitu hicho.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, zama za ubabe na utumiaji mabavu zimepitwa na wakati na kueleza bayana kwamba, Marekani haina ubavu wa kuanzisha muungano hata katika maeneo ambayo ina satuwa na ushawishi.
Dakta Zarif ameongeza kuwa, nchi moja baada ya nyingine zimekuwa zikijitoa na kujiweka kando kutokana na kuona aibu kuhesabiwa kuwa ziko katika faharasa ya nchi zilizoko pamoja na Marekani.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kujiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kutotekeleza ahadi madola ya Ulaya na kusema kuwa, Tehran itachukua hatua ya tatu ya kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA ambayo kimsingi inaendana na makubaliano hayo, na hatua hiyo haina maana ya kujitoa katika makubaliano hayo ya nyuklia.
Dakta Zarif amezungumzia pia mgogoro wa Yemen na kusema kwamba, njia ya utatuzi wa mgogoro huo ni mazungumzo.