Rwanda na DRC kushirikiana katika kukabiliana na Ebola
Serikali za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeazimia kushirikiana katika kukabiliana na ugonjwa hatari wa Ebola.
Waziri wa afya wa Rwanda Diane Gashumba na mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Pierre Kangudia wamekutana na kukubaliana kuimarisha udhibiti katika maeneo ya mpaka wa nchi hizo ili kukabiliana na safari za kuvuka mpaka na kuzuia kuenea kwa Ebola.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano wao uliofanyika mkoani Rubavu, kaskazini magharibi ya Rwanda unaopakana na mji wa Goma, mashariki mwa DRC, imesema nchi hizo mbili zimejitahidi kutumia njia za kudhibiti Ebola na kuhakikisha safari za mpakani ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa watu zaidi ya 1,700 wameaga dunia ndani ya miezi 11 iliyopita kutokana na ugonjwa hatari wa Ebola tangu uripuke upya nchini Kongo DR mwezi Agosti mwaka jana 2018.
Mfumuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa Afrika.