Zarif: Ugaidi wa kiuchumi wa Marekani walenga watu wa kawaida
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Ugaidi wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya nchi huru unalenga kuwadhuru watu wa kawaida."
Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameyasema hayo leo Ijumaa katika kujibu ujumbe wa Twitter wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba ambaye amelaani vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya taifa la Iran. Zarif ameandika katika akaunti yake ya Twitter kuwa: "Ugaidi wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya Cuba, China, Russia, Syria, Iran na wengineo unalenga kuwadhuru raia. Marekani inataka kufikia malengo yake haramu kwa kuwatisha watu wasio na hatia."
Zarif ameongeza kuwa, mbali na kuziwekea vikwazo nchini huru, Marekani pia inatekeleza uharamia, inatoa rushwa na inatumia vitisho na mabavu kufikia malengo yake. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ameishukuru Cuba kwa kuendelea kuiunga mkono Iran na kusisitiza kuwa: "Iran nayo iko pamoja na Cuba."
Siku ya Alhamisi, Bruno Rodriguez, Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba alituma ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter na kulaani vikwazo vya Marekani dhidi ya mashirika ya usafiri wa bahirini ya Iran na kusema vikwazo hivyo ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba ameongeza kuwa, hatua za Marekani za utumiaji mabavu na kuzuia kuuzwa mafuta ya Iran ni tishio kwa usalama na utulivu katika eneo lenye misukosuko la Asia Magharibi.
Ikumbukwe kuwa Jumatano, Marekani iliendeleza uraibu wake wa vikwazo kwa kutangaza kuwekea vikwazo watu, mashirika, na meli ambazo zina uhusiano na Iran.