Ayatullah Hamedani awataka Waislamu wa Kashmir waendeleze muqawama
Mwanachuoni mashuhuri hapa nchini Iran sambamba na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwaunga mkono Waislamu wanaodhulumiwa wa eneo la Kashmir, amewataka Wakashmir waendelee kusimama kidete na kudumisha moyo wa muqawama.
Ayatullah Hossein Noori-Hamedani mmoja wa marajii taqlidi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ametoa mwito huo leo Jumapili katika mji wa Qom, kusini mwa Tehran hapa nchini, katika mazungumzo yake na wanazuoni kadhaa wa eneo la Kashmir.
Ameeleza bayana kuwa, Waislamu wana jukumu la kuwa macho na kusimama kidete dhidi ya njama za maadui. Ayatullah Hossein Noori-Hamedani amefafanua kuwa, "India, Pakistan na Bangladesh zilikuwa eneo moja, lakini Waingereza waliliteganisha ili kuibua uhasama na mgawanyiko, na kusababisha hali ya sasa ya mpasuko katika eneo la Kashmir."
Msomi huyo wa Kiislamu hapa nchini ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitachoka kuwasaidia na kuwaunga mkono wanaodhulumiwa, sanjari na kusimama kidete dhidi mabeberu.
Mwezi uliopita wa Agosti, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alibatilisha mamlaka ya kujitawala eneo la Kashmir hatua ambayo Pakistan iliitaja kuwa kinyume cha sheria.
Mgogoro wa Kashmir ulianza wakati Pakistan na India zilipotengana mwaka 1947 baada ya kuondoka mkoloni Muingereza ambaye alipanda mbegu za chuki baina ya mataifa hayo mawili.