Oct 01, 2019 03:22 UTC
  • Rouhani: Iran inataka kuimarisha uhusiano na majirani zake

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inatoa kipaumbele katika siasa zake za kigeni suala la kuimarisha ushirikiano na majirani zake.

Rais Rouhani alisema hayo jana Jumatatu katika mazungumzo yake na mwenzake wa Armenia, Armen Sarkissian mjini Yerevan, alikoenda kushiriki mkutano wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya na Asia (EAEU).

Ameeleza bayana kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha kwa mikono miwili suala la kuimarisha ushirikiano na majirani zake." Ameongeza kuwa, kuleta amani ya kudumu na usalama katika eneo ni jambo lisiloepukika na kusisitiza kwamba ushirikiano jumuishi unahitajika ili kuweza kutatua migogoro ya eneo kwa njia ya amani.

Kuhusu uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Yerevan, Dakta Rouhani amesema nchi mbili hizi zinajivunia ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali za kiuchumi kama vile biashara, usafirishaji, mawasiliano, viwanda na nyinginezo, na kwamba kuna fursa ya kupanuliwa uhusiano huo.

Marais Rouhani na mwenzake wa Armenia, Armen Sarkissian wakiongoza mkutano wa pande mbili mjini Yerevan 

Amesisitiza kuwa, Iran ya Kiislamu iko tayari kuipa Armeni tajriba yake katika masuala ya uhandisi wa kiufundi, nishati na ujenzi wa mabwawa.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kadhalika amedokeza kuwa Tehran imejiunga na Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya na Asia (EAEU) kuanzia mwezi huu wa Oktoba, na kwamba hatua hiyo itafungua ukurasa mpya wa kuimarika miamala ya kibiashara na uchumi wa sekta za umma na binafsi za Iran.

Tags