Apr 24, 2016 06:53 UTC
  • Mazungumzo ya Zarif na Kerry; shaka juu ya mwenendo wa Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amesema nchi hiyo haitaziwekea vizuizi benki au mashirika ya kigeni yasifanye biashara na mashirika ya Iran ambayo hayakabilwi tena na vikwazo.

Baada ya mazungumzo aliyofanya siku ya Ijumaa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Muhammad Javad Zarif, Kerry aliyaeleza mashirika ya fedha ya kigeni kuwa kama yana swali lolote yatapata jawabu yake kwa maafisa wa Marekani. Aliongezea kwa kusema, mashirika hayo yasifikiri kwamba kile ambacho katika wakati fulani kilipigwa marufuku, mpaka sasa kingali ni marufuku. Aidha yasifikiri kuwa miamala ambayo ni marufuku kufanya na Iran kwa mashirika ya Marekani itakuwa marufuku pia kwa mashirika ya nje ya nchi hiyo.

Matamshi hayo ya John Kerry yamezusha maswali na tathmini tofauti kwa duru za habari na za kisiasa kuhusu makubaliano kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran.

Wafuatiliaji wa kadhia hiyo wanasema kutekelezwa ipasavyo makubaliano hayo ya nyuklia itakuwa ndiyo ithbati ya ukweli wa maneno ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani. Ushahidi unaonesha kuwa Marekani inafanya uafriti na kukwamisha utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia huku ikiwashinikiza pia waitifaki wake wa Ulaya wajitenge na Iran. Ni kutokana na mwenendo huo usio na muamana wa Washington ndipo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akasema, anatumai kuwa matamshi ya John Kerry yataweza kuondoa wasiwasi wa nchi za Ulaya kuhusiana na muelekeo wa Marekani.

Katika mazungumzo ya pamoja na waandishi wa habari aliyofanya na Federica Mogherini, wakati Mkuu huyo wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya alipofanya safari hivi karibuni hapa mjini Tehran, Zarif alisema kuna ulazima kwa pande zote na hasa Marekani kuheshimu ahadi zao, na si kwa maandishi tu bali kwa kuzitekeleza kivitendo na kuondoa vizuizi vilivyopo hususan katika sekta ya miamala ya kibenki.

Ukweli ni kwamba nchi nyingi za Magharibi ziko chini ya satua ya Marekani; na uhusiano wao na Iran umekabiliwa na matatizo kadhaa kutokana na taathira ya mashinikizo hayo ya Washington. Marietje Schaake, afisa wa bunge la Ulaya amezungumzia ukweli huo kwa kusema:"Ulaya imegeuka kuwa mateka wa Marekani. Sisi tulifanya mazungumzo kwa lengo la kufikia makubaliano ya nyuklia, lakini hivi sasa Marekani inakwamisha utekelezaji wake".

Baada ya kufikiwa makubaliano rasmi ya nyuklia, serikali ya Marekani iliibua na kuanza kuyafatilia masuala kadhaa kwa madhumuni ya kuishinikiza Iran. Siku ya Jumatano ya tarehe 20 mwezi huu, Mahakama Kuu ya Marekani ilipitisha uamuzi kuwa katika kuchunguza madai ya waathirika wa eti makosa ya jinai za ugaidi mahakama za nchi hiyo zinaweza kutumia mali na fedha za Iran zilizozuliwa nchini humo ili kuwalipa fidia watu hao .

Matamshi ya John Kerry yanathibitisha ukweli huu, kwamba licha ya kufikiwa makubaliano ya nyuklia, Marekani inatekeleza siasa za kiafriti na ukwamishaji dhidi ya Iran. Kerry alieleza kwamba vikwazo vilivyosalia vya Marekani dhidi ya Iran kwa sababu ya majaribio ya makombora ya balastiki pamoja na rekodi ya huko nyuma ya Tehran kuhusiana na haki za binadamu na kufadhili ugaidi ndiyo sababu pekee inayozifanya pande za kigeni zisiwe na hamu ya kufanya miamala ya kibiashara na Iran; na hata akadai kwamba mwenendo wa Tehran umewafanya wafanyabiashara wawe na shaka na hatihati ya kuingia kwenye soko la Iran.

Kutokana na muelekeo hasi wa serikali ya Marekani dhidi ya Iran na shaka zilizopo kuhusiana na mwenendo wa nchi hiyo, wadadisi wa mambo wanahisi kuwa, ni vigumu kuamini kwamba serikali ya Obama itachukua hatua zaidi za kujenga hali ya kuaminiana.

Kwa sababu hiyo kuna ulazima wa kutathminiwa kwa makini na kwa karibu mwenendo wa Washington kupitia mawasiliano na mazungumzo ya kidiplomasia ya ngazi za juu katika Umoja wa Mataifa kuanzia New York, Geneva mpaka Vienna. Ni wazi kuwa kuendeleza Marekani hatua zake za kiafriti kunaweza kusababisha matatizo katika utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia.

Iran na nchi zote zinazounda kundi la 5+1 zimeteua timu ya waratibu wa kushughulikia suala hilo; hivyo kuna haja ya kuundwa tume itakayohakikisha makubaliano ya nyuklia yanatekelezwa ipasavyo. Na ndiyo maana wakati Zarif na Kerry walipokuwa wakikutana mjini New York, huko Vienna pia kilifanyika kikao cha manaibu waziri wa mambo ya nje wa Iran na wa kundi la 5+1.../

Tags