Kamanda wa Jeshi la Anga la Iran: Tumetungua ndege isiyo na rubani ya nchi ya kigeni
(last modified Sat, 09 Nov 2019 03:15:11 GMT )
Nov 09, 2019 03:15 UTC
  • Kamanda wa Jeshi la Anga la Iran: Tumetungua ndege isiyo na rubani ya nchi ya kigeni

Kamanda wa Jeshi la Anga la Iran amesema kuwa jeshi hilo limetungua ndege isiyo na rubani ya nchi ya kigeni baada ya kuingia katika anga ya kusini mwa Iran katika eneo la Mahshahr.

Brigedia Jenerali Alireza Sabahi-Fard amesema kuwa, hatua hiyo imechukuliwa baada ya ndege hiyo isiyo na rubani kuingia kinyume cha sheria katika anga ya Iran na kwamba ndege hiyo ilitunguliwa kabla ya kufika katika maeneo nyeti ya muhimu.  

Brigedia Jenerali Sabahi-Fard ameongeza kuwa, kikosi cha anga cha jeshi la Iran kiko tayari kwa ajili ya kukabiliana na uchokozi wa aina yoyote katika anga ya nchi hii. 

Alfajiri ya jana Ijumaa wakazi wa bandari ya Mahshahr katika mkoa wa Khuzestan huko kusini mwa Iran walisikia sauti za milipuko na baadaye ilibainika kuwa milipuko hiyo ilitokana na kutunguliwa ndege isiyo rubani ya nchi ya kigeni iliyoingia Iran kinyume cha sheria. 

Mji wa bandarini wa Mahshahr una eneo kubwa zaidi la kiuchumi la petrokemikali katika Mashariki ya Kati na bandari ya Imam Khomeini ambayo ni miongoni mwa bandari kubwa zaidi hapa nchini iko katika wilaya hiyo. Eneo hilo la Mahshahr limekuwa likifuatiliwa sana na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na nafasi yake muhimu katika uchumi wa Iran.  

Tags