Iran, Afrika Kusini kushirikiana kuinua hadhi ya wanawake
(last modified Mon, 25 Apr 2016 04:04:35 GMT )
Apr 25, 2016 04:04 UTC
  • Iran, Afrika Kusini kushirikiana kuinua hadhi ya wanawake

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya wanawake Bi. Shahindokht Molaverdi amesema, Iran na Afrika Kusini zitashirikiana katika kuinua hadhi ya wanawake.

Aliyasema hayo jana Jumapili hapa mjini Tehran alipokutana na kufanya mazungumzo na Bi. Bongi Ngema-Zuma, mke wa Rais wa Afrika Kusini aliyeko safarini hapa nchini Iran.

Bi. Molaverdi amesema, serikali ya Iran inalipa kipaumbele suala la ustawi na uwezo wa wanawake na kuongeza kuwa: "Hivi sasa tunafuatilia suala la kuimarisha uwezo wa wanawake kote nchini Iran na kwa hivyo kubadilishana mawazo na Afrika Kusini kuhusu suala hili kutatoa msaada mkubwa kwa wanawake."

Kwa upande wa Bi. Bongi Ngema-Zuma amesema, wakati wanawake wanapokuwa na uwezo, taifa nalo hupata uwezo.

Aidha amesema, serikali ya Afrika Kusini imechukua hatua mbalimbali za kuleta usawa wa kijinsia na kwamba baada ya kuangua mfumo wa ubaguzi wa rangi, wanawake Afrika Kusini wameshuhudia ustawi mkubwa.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini aliwasili Tehran jana Jumapili akiongoza ujumbe wa watu 180 wakiwemo maafisa wa serikali na wawekezaji. Rais Zuma anatembelea Iran kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake Rais Rouhani ili kujadili masuala ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika nyuga tofauti.

Marais hao jana walikutana katika Ikulu ya Saadabad, na kujadiliana njia za kuimarisha uhusiano wa pande mbili, mbali na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa.

Tags