Tehran; kituo cha udiplomasia wa kisiasa-kiuchumi wa nchi zinazopakana na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i57695-tehran_kituo_cha_udiplomasia_wa_kisiasa_kiuchumi_wa_nchi_zinazopakana_na_iran
Tehran, mji mkuu wa Iran, katika kipindi cha wiki moja iliyopita, umekuwa mwenyeji wa mawaziri wa nchi jirani za ukanda wa kusini na kaskazini. Aidha katika siku za hivi karibuni mji wa Tehran umekuwa mwenyeji wa mikutano kadhaa ya kieneo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 05, 2019 07:30 UTC
  • Tehran; kituo cha udiplomasia wa kisiasa-kiuchumi wa nchi zinazopakana na Iran

Tehran, mji mkuu wa Iran, katika kipindi cha wiki moja iliyopita, umekuwa mwenyeji wa mawaziri wa nchi jirani za ukanda wa kusini na kaskazini. Aidha katika siku za hivi karibuni mji wa Tehran umekuwa mwenyeji wa mikutano kadhaa ya kieneo.

Ushirikiano na nchi jirani ni kipaumbele katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ni katika fremu hii ndio wakuu wa Iran wakalipa umuhimu mkubwa suala la kufuatilia uimarishwaji ushirikiano na mataifa jirani. Kwa kuzingatia uwezo mkubwa wa kiuchumi wa nchi jirani, ukuruba wa kijiograjifa na nukta za pamoja za kiutamaduni, kidini na kilugha baina ya Iran na majirani zake, kuna udharura wa kuimarishwa zaidi uhusiano na nchi hizo.

Kwa kuzingatia soko kubwa katika nchi zinazopakana na Iran katika pande za kaskazini, kusini, mashariki na magharibi, wazalishaji bidhaa na wafanybiashara nchini  wanaweza kuingia katika masoko hayo na kukidhi mahitaji ya nchi hizo kwa kuuza bidhaa zenye kiwango cha juu.

Waziri wa Nishati wa Iran na Waziri wa Maji wa Syria

Ni kwa msingi huo ndio kukafanyika Kongamano la Iran na Eurasia siku ya Jumapili mjini Tehran. Baada ya Iran kujiunga na Jumuiya ya Kiuchumi ya Eurasia, kumejitokeza fursa mpya ambazo zinaweza kutumiwa na wafanyabiashara na mashirika ya uzalishaji bidhaa nchini Iran ili yaweze kuingia katika soko la nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Lengo la kufanyika Kongamano la Iran na Eurasia mjini Tehran ni kuyawezesha mashirika ya Iran kuzifahamu nchi wanachama wa jumuiya hiyo ya kiuchumi ambayo kwa ujumla ina soko la pamoja la watu takribani milioni 200. Korido ya kimatiafa ya uchukuzi ya kuunganisha kaskazini na kusini inaweza kufanikishwa kwa ushirikiano wa Iran na Jumuiya ya kiuchumi ya Eurasia.

Reza Ardakanian, Waziri wa Nishati wa Iran, akizungumza pembizoni mwa Kongamano la Iran na Eurasia ameashiria kuundwa jumuiya za  ushirikiano wa kieneo na kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na vikwazo vya kiuchumi na kusema: "Uanachama wa Iran katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Eurasia ni mfano wa wazi wa kubadilisha vikwazo kuwa fursa.

Mbali na mkutano huo wa Iran na Eurasia, Alhamisi hii Tehran ni mwenyeji wa Kikao cha 10 cha Baraza la Kieneo la Usimamizi wa Maji ya Miji. Kikao hicho ni katika fremu ya kufuatilia maslahi ya kitaifa ya Iran katika uga wa udiplomasia wa maji, mito ya mpakani, vyanzo vya pamoja na maji na kuarifisha huduma za kiufundi na kiuhandisi za Iran katika uga wa maji. Kwa maneneo mengine ni kuwa, kikao hicho kinaweza kuandaa mazingira kwa mashirika ya Iran kufanya kazi katika nchi jirani katika uga mpana wa maji.

Kwa mfano, Iran sasa imefikia mapatano na Syria kuhusu njia za ushirikiano wa nchi mbili katika kuwezesha mashirika ya Iran kuanza kufanya kazi katika sketa ya maji na nishati katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Katika uga huo, Reza Ardakanian, Waziri wa Nishati wa Iran siku ya Jumatano alikutana na Waziri wa Maji wa Syria na kusema: "Mashirika ya Iran yatashiriki katika ukarabati wa mtandao wa maji safi na maji taka nchini Syria.

Kikao cha 10 cha Baraza la Kieneo la Usimamizi wa Maji ya Miji mjini Tehran

Aidha wiki hii Tehran imekuwa mwenyeji wa Yusuf Bin Alawi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Shahin Mustafayev Waziri wa Uchumi wa Azerbaijan, Uthman Ali Uthmanzadeh, Waziri wa Nishati wa Tajikistan  na Sanjar Makanbatov pamoja na Janat Bishnov mawaziri wa uchumi na uchukuzi wa Kyrgyzstan. Kwa msingi huo wiki hii mji mkuu wa Tehran umekuwa kituo cha udiplomasia na nchi jirani. Sisistizo kuhusu amani na utulivu katika eneo kwa lengo la kudhamini maslahi ya nchi za eneo na jirani ni ujumbe muhimu wa mazungumzo hayo ambayo yamefanyika mjini Tehran.