Watu 16,000 wajisajili kugombea ubunge Iran, ongezeko la 29%
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i57756-watu_16_000_wajisajili_kugombea_ubunge_iran_ongezeko_la_29
Mwenyekiti wa Makao Makuu ya Uchaguzi nchini Iran amesema watu 16,000 wamejiandikisha kwa ajili ya kugombea ubunge katika uchaguzi ujao hapa nchini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 08, 2019 09:26 UTC
  • Watu 16,000 wajisajili kugombea ubunge Iran, ongezeko la 29%

Mwenyekiti wa Makao Makuu ya Uchaguzi nchini Iran amesema watu 16,000 wamejiandikisha kwa ajili ya kugombea ubunge katika uchaguzi ujao hapa nchini.

Jamal Orf amesema hayo leo Jumapili katika kikao na waandishi wa habari hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, idadi hiyo inaashiria ongezeko la asilimia 29 ya wagombea walionyesha hamu ya kuwania ubunge, ikilinganishwa na duru zilizopita za usajili.

Mchakato wa kuwasajili wagombea hao wa uchaguzi wa awamu ya 11 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ulianza Disemba Mosi na kumalizika jana Jumamosi ya Disemba 7.

Bunge la Iran

Uchaguzi wa Bunge la Iran umepangwa kufanyika Februari 21 katika maeneobunge 208 kote Iran kwa ajili ya kuwachagua wabunge 290. Uchaguzi wa mwisho wa ubunge ulifanyika hapa nchini mwaka 2016.

Mwenyekiti wa Makao Makuu ya Uchaguzi nchin Iran ameongeza kuwa, watu 81 wamejiandikisha pia kwa ajili ya kuwania nafasi ya wajumbe wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu.