Iran inapinga kutumiwa haki za binadamu kama chombo cha kisiasa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa jibu kwa taarifa ya Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya na kusema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga kutumiwa haki za binadamu kama chombo cha kisiasa dhidi ya nchi huru na zenye kujitegemea."
Siku ya Jumapili, mkuu mpya wa sera za kigeni katika Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, alitoa taarifa ya uingiliaji na kuituhumu Iran kuwa eti inakiuka haki za binadamu katika kukabiliana na wapinzani.
Akijibu kauli hiyo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Sayyid Abbas Mousavi amebainisha masikitiko yake kuwa mkuu mpya wa sera za kigeni katika Umoja wa Ulaya ametoa taarifa yake hiyo kutokana na taarifa ghalati na zisizo sahihi alizozipokea. Mousavi amesisitiza kuwa, kuzingatia haki za binadamu ni msingi wa lazima katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inazingatia utawala wa wananchi waliowengi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Utendaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha miongo minne iliyopita umeonyesha namna nchi hii inavyolipa uzito suala la haki za binadamu.
Aidha amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wananchi wana haki ya kujumuika kwa amani na kubainisha malalamiko yao.
Mousavi ameendelea kusema kuwa: "Umoja wa Ulaya unapaswa kuzingatia kwa kina ukiukwaji wa haki za binadamu katika baadhi ya nchi wanachama wa umoja huo au waitifaki wa umoja huo." Aidha ameutaka Umoja wa Ulaya utekeleze ahadi zake katika mapatano ya nyuklia ya Iran na ukabiliane na ukiukwaji wa haki za watu milioni 80 wa Iran ambao haki zao zimekiukwa kutokana na athari za vikwazo vilivyo dhidi ya ubinadamu na vya upande mmoja vya Marekani.