Zarif: Kuna udharura kuchukua hatua za pamoja kukabiliana na vikwazo vya Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito kwa jamii ya kimataifa ichukue hatua za kukabiliana na sera za Marekani za kutumia vikwazo ambazo amesema zimefika kiwango cha uraibu.
Mohammad Javad Zarif katika ujumbe wake kupitia Twitter Jumapili usiku ameashiria 'uraibu wa Marekani wa vikwazo' na kuongeza kuwa, kukabiliana na vikwazo vya Marekani ni jambo ambalo linahitaji azma na hatua za pamoja.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kuandika kuwa : "Marekani ina ugonjwa wa uraibu wa vikwazo na hali hiyo inawaathiri marafiki na pia maadui wa Washington."
Katika miezi ya hivi karibuni, mbali na kuwa Marekani imekithirisha vikwazo dhidi ya nchi ambazo ni mahasimu wake, imeanza pia kuziwekea vikwazo nchi waitifaki.

Katika bajeti yake ya kijeshi ya mwaka 2020, si tu kuwa Marekani imetoa vitisho dhidi ya Iran, Russia, Korea Kaskazini na China bali pia imetoa vitisho kwa nchi waitifaki kama vile Uturuki na nchi za Ulaya.
Aidha Marekani imetoa vitisho vya vikwazo kwa washirika wake wengine kama vile India na Misri kutokana na nchi hizo kuamua kununua silaha kutoka Russia.