Iran: "Muamala wa Karne" ni "Usaliti wa Karne"
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, mpango wa ulazimishaji wa Marekani uitwao Muamala wa Karne ni Usaliti wa Karne dhidi ya haki za watu wa Palestina; na akasisitiza kuwa, mpango huo wa amani wa kuaibisha na wa ulazimishaji wa Marekani kwa Wapalestina utafeli na kugonga mwamba tu.
Sayyid Abbas Mousavi ameuelezea mpango huo wa amani wa ulazimishaji wa Marekani uitwao "Muamala wa Karne" kuwa ni "Usaliti wa Karne" dhidi ya haki za watu wa Palestina na umma wa Kiislamu na ametoa mwito kwa nchi na mataifa yenye fikra huru katika eneo na duniani kote kukabiliana na mpango huo wa kuaibisha.
Msemaji wa Wizara ya Mamboya Nje ya Iran ameashiria kuwa, ardhi ya Palestina ni milki ya watu wa Palestina na akabainisha kwamba: Utawala wa Kizayuni ni utawala ghasibu unaokalia ardhi kwa mabavu; na njia pekee ya kutatua mgogoro wa Palestina ni kuitishwa kura ya maoni itakayoshirikisha wakaazi wa asili wa ardhi ya Palestina na kwamba mipango ya kihabitihi kama huo wa Marekani itafeli tu.
Mousavi amesema, kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, suala la Palestina na Quds tukufu ni suala la kipaumbele cha kwanza kwa Ulimwengu wa Kiislamu na akaongeza kuwa, inasikitisha kuona baadhi ya nchi za Kiislamu zimelipuuza lengo hilo tukufu linalogusa heshima ya Waislamu na nchi za Kiislamu, zimemfanya adui kuwa rafiki na zimepuuza kwa makusudi au kwa mghafala jinai dhidi ya binadamu za miaka zaidi ya 70 zilizofanywa na utawala wa Kizayuni.
Rais Donald Trump wa Marekani jana alichukua hatua ya upande mmoja na bila kujali kugonga mwamba juhudi zake za miezi kadhaa za kutafuta uungaji mkono wa kieneo na kimataifa pamoja na ridhaa ya mirengo ya Palestina, kwa kuamua kuzindua mpango wa Kizayuni alioupa jina la "Muamala wa Karne".
Mpango huo unaokidhi matakwa ya utawala haramu wa Israel na kufuta haki za wananchi madhulumu wa Palestina umeandaliwa na serikali ya Marekani kwa ushirikiano na maafikiano na baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia, Bahrain na Imarati.../