Iran yazindua kombora jipya la 'Raad 500'
Iran imezindua kombora jipya linalojulikana kama 'Raad 500' ambalo linatumia injini aina ya kompositi inayojulikana kama 'Zahir' sambamba na kuzindua kizazi kipya cha makombora ya kijeshi na makombora ya kubeba satalaiti. Uzinduzi huo umehudhuriwa na Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Meja Jenerali Hussein Salami.
Kwa mujibu wa tovuti ya Sepah News, katika hafla hiyo pia kumezinduliwa kizazi kipya cha injini aina ya kompositi ya anga za mbali inayojulikana kama 'Salman' ambayo itatumika katika makombora ya kijeshi na makombora ya kubeba satalaiti.
Mafanikio hayo yataiwezesha Iran kutengeneza makombora ya kubeba satalaiti yenye uzito wa chini na pia makombora ya nchi kavu kwa nchi kavu na nchi kavu kwa anga. Hali kadhalika teknolojia mpya iliyotumika inawezesha makombora hayo ya Iran kukwepa ngao za makombora zinazotumiwa na adui.

Mafanikio ya Iran katika sekta ya ulinzi na kujihami yanaendelea kutoa indhari kwa madola ya kigeni yanayofanya chochoko dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kadiri Iran inavyopiga hatua kubwa katika sekta hiyo ndivyo maadui wake wanavyozidi kufeli na kudhoofika. Iran imefanikiwa katika sekta ya kijeshi pamoja na kuwa imewekewa vikwazo ambavyo havijawahi kushuhudiwa dhidi ya nchi yoyote ile.