Rouhani: Uingiliaji mambo wa Marekani unahatarisha usalama na uthabiti wa eneo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60653-rouhani_uingiliaji_mambo_wa_marekani_unahatarisha_usalama_na_uthabiti_wa_eneo
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya Marekani ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi za Asia Magharibi imevuruga usalama na uthabiti katika eneo hili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 28, 2020 02:50 UTC
  • Rouhani: Uingiliaji mambo wa Marekani unahatarisha usalama na uthabiti wa eneo

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya Marekani ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi za Asia Magharibi imevuruga usalama na uthabiti katika eneo hili.

Rais Rouhani alisema hayo jana Jumatatu katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa China, Xi Jinping, na kueleza bayana kuwa, "dunia hivi sasa ipo katika hali ambayo, kila mmoja anahitaji usaizidi wa mwingine, lakini kuna baadhi ya mataifa yanashupalia vikwazo vyao haramu na vya kikatili."

Sambamba na kuishukuru China kwa kupinga vikwazo hivyo haramu vya Marekani dhidi ya Iran, Rais Rouhani amesema hatua madhubuti za nchi kama China ndizo zitakazoifanya dunia iondokane na vikwazo.

Dakta Rouhani amebainisha kuwa, "usalama wa eneo hili na njia zake za bahari una umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Iran, lakini kwa bahati mbaya nyendo hatarishi za Marekani huenda zikavuruga uthabiti katika eneo la Ghuba ya Uajemi."

Rais Jinping mbali na kuishukuru Tehran kwa misaada yake kwa watu wa China mwanzoni mwa janga la Corona, amelaani hatua ya Marekani ya kuendelea kuliwekea taifa hili vikwazo na kushupalia sera yake ya mashinikizo ya kiwango cha juu, katika hali ambayo aghalabu ya nchi zinataka migogoro ipatiwe ufumbuzi wa kisiasa.

Dkt Rouhani na Rais wa Croatia

Katika hatua nyingine, Rais Zoran Milanović wa Croatia ambaye hivi sasa ni mwenyekiti wa kiduru wa Baraza la Umoja wa Ulaya, amekosoa vikali hatua ya Marekani kushadidisha vikwazo vyake dhidi ya Iran wakati huu wa kupambana na janga la Corona.

Katika mazungumzo ya simu na Dakta Rouhani hapo jana, Milanović alieleza kusikitishwa kwake na kitendo hicho cha Washington kuongeza vikwazo visivyo vya kibinadamu dhidi ya taifa la Iran wakati huu wa mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19.