Kiongozi Muadhamu asisitiza kuhusu umuhimu wa wafanyakazi katika uchumi salama
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60815-kiongozi_muadhamu_asisitiza_kuhusu_umuhimu_wa_wafanyakazi_katika_uchumi_salama
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuhusu nafasi na umuhimu wa wafanyakazi na majukumu ya mwajiri na mwajiriwa katika kuimarisha ubora na wingi wa uzalishaji na utajiri katika uchumi salama.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 06, 2020 11:32 UTC
  • Kiongozi Muadhamu asisitiza kuhusu umuhimu wa wafanyakazi katika uchumi salama

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuhusu nafasi na umuhimu wa wafanyakazi na majukumu ya mwajiri na mwajiriwa katika kuimarisha ubora na wingi wa uzalishaji na utajiri katika uchumi salama.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo Jumatano kwa mnasaba wa Wiki ya Wafanyakazi  ambapo alikuwa na mawasiliano ya moja kwa moja ya video na viwanda saba. Kiongozi Muadhamu ametuma salamu zake za kheria na fanaka kwa wafanyakazi wote kwa mnasaba wa Wiki ya Wafanyakazi na kusema amevutiwa na ripoti zenye kuleta matumaini kuhusu uzalishaji. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuhusu kutangazwa ripoti hizo kwa umma na kusema kutatua matatizo ya wafanya kazi ni kati ya masuala  muhimu ambayo yanapaswa kuzingatiwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema lengo la uchumi wa nchi ni kuzalisha utajiri na kisha kuugawa kwa uadilifu baina ya wananchi na kuongeza kuwa: "Ili kufika katika uchumi salama, mfanyakazi ni moja ya nguzo kuu na mhusika wa daraja la kwanza katika uzalishaji utajiri katika nchi."

Ayatullah Khamenei amesema mfanyakazi mahiri na mwenye ubunifu hupelekea kuongezeka ubora wa kazi na kuongeza kuwa: "Kwa msingi huo mashirika ya kiuchumi na waajiri wanapaswa kuimarisha ujuzi wa wafanyakazi, ili kuongeza rasilimali ya mashirika. Wafanyakazi nao wanapaswa kuwajibika na wafanye kazi bila kuzembea."

Kiongozi Muadhamu amesema waajiri na waajiriwa ni nguzo mbili muhimu katika ustawi wa kiuchumi na amesisitiza kuhusu haki za wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuwapa mshahara adilifu na kuwalipa kwa wakati bila kuchelewa, kuwapa usalama wa ajira, bima, mafunzo ya kikazi, huduma za kijamii na kiafya.

Kiongozi Muadhami wa Mapinduzi ya Kiislamu akishuhudia ustawi wa Iran katika uzalishaji kwa njia ya video

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu  ameendelea na hotuba yake kwa kuashiria maudhui ya ' Ustawi Mkubwa katika Uzalishaji' ambayo ni nara na kauli mbiu ya mwaka huu wa 1399 Hijria Shamsia (ulioanza Machi 21 2020) na kusema: "Uzalishaji katika uchumi wa Iran ni sawa na mfumo wa kinga katika mwili wa mwanadamu; kama ambavyo mfumo wa kinga mwilini una umuhimu mkubwa katika kukabiliana na virusi, iwapo uzalishaji utakuwa ni wa kiwango kizuri na wenye kustawi, basi uchumi wa nchi unaweza kukabiliana na virusi vya kimaumbile na vya kubuniwa kama vile vikwazo na kujikinga na misukosuko katika bei ya mfuta na matatizo mengine mbali mbali.

Kiongozi Muadhamu amesema kuunga mkono uzalishaji na wazalishaji ni kati ya majukumu ya msingi ya wakuu wa nchi na kuongeza kuwa: "Kuunga mkono uzalishaji hakumaanishi tu kutoa msaada ya kifedha bali kunajumuisha pia kuondoa vizingiti na kufungua medani kwa ajili ya wawekezaji, wanafikra na wazalishaji."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria baadhi vizingiti vinavyopaswa kuondolewa na kusema: "Kuondolewa urasimu wenye kuzuia mambo kusonga mbele, kukabiliana kwa nguvu na ulanguzi wa bidhaa, kukabiliana na uagizaji kiholela wa bidhaa kutoka nje ya nchi, kukabiliana na ufisadi wa kifedha na kiidari, kuzingatia haki miliki, kukabiliana na wenye kuvuruga masoko, na pia kutoa ruzuku ya ushuru panapohitajika ni nukta ambazo zinapaswa kuzingatiwa na kutekelezwa na mihimili mitatu ya dola."

Katika ujumbe wake kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa 1399 Hijria Shamisia, Kiongozi Muadhamu aliutaja mwaka huu kuwa Mwaka wa Ustawi Mkubwa katika Uzalishaji .