Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu; Uzalishaji, msingi wa kujengea uchumi imara
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, uzalishaji ndio msingi unaowezesha kupatikana uchumi wa kitaifa na ulio imara.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alitoa sisitizo hilo jana alipozungumza mubashara kwa njia ya vidio na taasisi saba za uzalishaji nchini kupitia hotuba aliyotoa kwa mnasaba wa Wiki ya Kazi na Mfanyakazi.
Ayatullah Khamenei alibainisha kuwa, kama ambavyo nafasi ya mfumo wa kinga ya mwili ni muhimu sana katika kukabiliana na virusi, ikiwa uzalishaji utakuwa wa kiwango kizuri na wenye kustawi, utaweza kuulinda mwili wa uchumi wa nchi na virusi vya matukio ya kimaumbile na virusi vya kutengenezwa kama vikwazo au ushukaji wa bei ya mafuta na mitikisiko mingine tofauti.
Kwa kuzingatia kuwa uzalishaji wa ndani una nafasi kadhaa kimchango katika kujenga uwezo na nguvu, ni kitu chenye umuhimu maradufu kwa kila nchi. Kadiri uchumi wa taifa unavyostawi na kuwa imara, ndivyo taathira yake katika nyuga tofauti za ndani na nje ya nchi zinavyoonekana zaidi.
Uzalishaji una uhusiano wa moja kwa moja na uchumi imara na unaoendana na mazingira; na kwa upande wa kiutamaduni, kijamii na hata kisiasa unaonyesha athari zake katika jamii ya ndani na ya mazingira yaliyoizunguka. Wakati mahitaji ya msingi ya wananchi na ya sekta ya viwanda na ufundi yanapozalishwa ndani ya Iran, huandamana na kujengeka moyo wa kujiamini na hisia za kuwa na izza na fahari; kwa sababu huwa ni kinga ya kuihifadhi nchi na mitikisiko ya kimataifa pamoja na nyenzo za vikwazo na mashinikizo ya kisiasa ya nje.
Zaidi ya hayo, hupelekea kupatikana pia uzalishaji wenye kiwango bora, uchumi wenye kustawi na unaoendana na mazingira pamoja na huduma bora kwa umma katika upeo wa jamii. Kwa kuongezeka uzalishaji na kukidhiwa mahitaji ya ndani, ndipo suala la usafirishaji na uuzaji bidhaa nje ya nchi linapokuwa na umuhimu, ambayo ni nembo ya kutangaza utamaduni na teknolojia za bidhaa za Kiirani kwa nchi zingine duniani.
Kwa kutoa mfano; katika kilele cha vita vya kupambana na corona na katika mwaka huu uliopewa jina la 'Mwaka wa Kasi Kubwa ya Uzalishaji' mashirika ya Kiirani ya elimu za kitaalamu (knowledge-based) yamefanya hima na juhudi kubwa na kuchapa kazi kwa kiwango maradufu kwa kuweza kuzalisha vifaa vya kukidhi mahitaji muhimu ya kitiba kwa ajili ya kukabiliana na kirusi hicho angamizi; na hivi sasa uzalishaji wake umefikia kiwango cha kusafirisha vifaa hivyo nje ya nchi. Shehena ya kwanza ya vifaa elfu 40 vya kupimia ugonjwa wa Covid-19 vilivyotengezwa na shirika moja la Kiirani la elimu za kitaalamu ilisafirishwa siku ya Jumanne kuelekea Ujerumani.
Yasha Farrokhzad, Mkurugenzi wa Masoko wa shirika la Kiirani la elimu za kitaalamu la "Pishtaz Teb" amesema: Kwa hima na juhudi za wanasayansi vijana wa Kiirani vimetengezwa vifaa venye ubora wa kiwango cha juu kabisa vya kupimia Copvid-19; na kwa sasa kuna nchi zaidi ya 60 ambazo zinataka zipatiwe vifaa vya shirika hili vinavyohusiana na corona.
Kuongezeka uzalishaji wenye kiwango kinachoendana na teknolojia na utaalamu wa kisasa duniani, mbali na kulipa msukumo gurudumu la uchumi wa taifa na kulifanya liwe imara, ni kielezo muhimu pia cha kuukinga uchumi wa Iran na kila aina ya virusi, kikiwemo kirusi cha vikwazo.
Kukidhi mahitaji muhimu na ya dharura ya wananchi na ya sekta ya viwanda na ufundi kwa kutegemea uzalishaji wa ndani, kutaufanya uchumi uwe salama na kuleta utulivu ndani ya jamii. Hivi sasa uhamasishaji unaofanywa wa kuzalisha na kukidhi mahitaji ya msingi ya kitiba kwa ajili ya kupambana na corona, zikiwemo barakoa, vifaa vya kupimia pamoja na vifaa vya kupumulia umeufanya uzalishaji wa ndani uwe na umuhimu maradufu na kuongeza nguvu na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.../