Rais Rouhani: Bunge la Iran ni nembo ya demokrasia ya kidini
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema bunge ni nembo ya demokrasia kote duniani, lakini ni nembo ya demokrasia ya kidini katika Jamhuri ya Kiislamu.
Rais Rouhani amesema hayo katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Bunge la 11 la Iran leo Jumatano na kuongeza kuwa, uhuru wa mihimili mitatu ya utawala haumaanishi kuweko mizozo baina ya taasisi hizo.
Huku akiwapongeza wabunge wapya wa Bunge hilo, Rais wa Iran amesema: Muhula wa kuhudumu serikali na Wabunge ni mfupi, lakini kwa ushirikiano baina ya mihimili hiyo miwili, kunaweza kukabakia athari chanya kwa miongo au hata kwa karne nyingi.
Amewaasa wabunge kutoa kipaumbele kwa masuala yenye maslahi ya taifa badala ya maslahi ya vyama na mirengo na kusisitiza kwamba hatua hiyo italifanya Bunge liwe 'jumba la taifa.'
Dakta Rouhani ameeleza bayana kuwa: Serikali haitaki Bunge linalopuuza majukumu yake ya kutunga sheria na usimamizi, lakini inataka Bunge lenye nguvu na ambalo kama alivyoeleza leo Kiongozi Muadhamu kwenye ujumbe wake, litakuwa ni chanzo cha matumaini kwa taifa na linaloweza kutegemewa na serikali.
Katika ujumbe uliosomwa katika Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bujge la Iran) na Mkuu wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatulislam Mohammadi Golpayegani katika ufunguzi wa duru ya 11 ya Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu leo Jumatano, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameitaka taasisi hiyo kujikita zaidi katika masuala ya uchumi wa kimuqawama na utamaduni.