Iran: Utawala wa Kizayuni ujiunge haraka na mkataba wa nyuklia wa NPT
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i64745-iran_utawala_wa_kizayuni_ujiunge_haraka_na_mkataba_wa_nyuklia_wa_npt
Mjumbe na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika taasisi za kimataifa zenye makao yao mjini Vienna, Austria ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ujiunge haraka na Mkataba za Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Nyuklia NPT, tena bila ya masharti yoyote.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 20, 2020 09:08 UTC
  • Iran: Utawala wa Kizayuni ujiunge haraka na mkataba wa nyuklia wa NPT

Mjumbe na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika taasisi za kimataifa zenye makao yao mjini Vienna, Austria ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ujiunge haraka na Mkataba za Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Nyuklia NPT, tena bila ya masharti yoyote.

Kazem Gharib Abadi ametoa mwito huo leo Ijumaa mjini Vienna, Austria na kusema kuwa, kitendo cha jamii ya kimataifa cha kufumbia macho silaha za nyuklia zinazomilikiwa na utawala dhalimu wa Israel ni hatari kwa usalama wa dunia nzima.

Amesema, jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuilazimisha Israel ijiunge haraka na mkataba wa NPT tena bila ya masharti yoyote.

 

Mbali na kusisitiza mara kwa mara kwamba, jamii ya kimataifa haina njia nyingine isipokuwa kuuweka chini ya mashinikizo utawala ghasibu wa Kizayuni ili ujiunge haraka na NPT, ameelezea kusikitishwa kwake na kuona kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel ndio pekee ambao si mwanachama wa NPT katika eneo la Asia Magharibi licha ya kujilimbikizia silaha hatari za mauaji ya halaiki ya watu.

Mwakilishi huyo wa kudumu wa Iran katika taasisi za kimataifa zenye makao yao huko Vienna Austria ameelezea pia wasiwasi wake kutokana na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu  yaani Imarati, kutoheshimu vipengee vya NPT na kuongeza kuwa, Saudi Arabia inafanya ukaidi wa kutotekeleza inavyotakiwa vipengee vya mkataba wa kupambana na silaha za nyuklia wa NPT huku Imarati nayo hadi hivi sasa haijatoa msimamo wowote rasmi wa kuheshimu kikamilifu vipengee vya mkataba huo.