Iran yataka Baraza la Usalama la UN lichunguze mauaji ya Fakhrizadeh
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i64914-iran_yataka_baraza_la_usalama_la_un_lichunguze_mauaji_ya_fakhrizadeh
Naibu Waziri wa Sheria wa Iran ametoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchunguza mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran shahidi Mohsen Fakhrizadeh.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 29, 2020 08:50 UTC
  • Iran yataka Baraza la Usalama la UN lichunguze mauaji ya Fakhrizadeh

Naibu Waziri wa Sheria wa Iran ametoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchunguza mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran shahidi Mohsen Fakhrizadeh.

Mahmoud Abbasi, Naibu Waziri wa Sheria wa Iran anayeshughulikia haki za binadamu na masuala ya kimataifa amesisitiza kuwa, oparesheni ya kigaidi iliyopelekea kuuawa Fakhrizadeh ni ukiukwaji wa mamlaka ya kujitawala na ni hujuma dhidi ya nchi.

Ameongeza kuwa kuuawa shahidi Mohsen Fakhrizadeh ambaye alikuwa Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu katika Wizara ya Ulinzi ya Iran ni kitendo cha hujuma dhidi ya Iran na hivyo Iran ina haki ya kulipiza kisasi.

Abbasi amesema ugaidi unaotendwa na mtu binafsi au serikali ni jinai ya kimataifa ambayo wahusika wake wanaweza kushtakiwa katika taasisi za kimataifa likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Jana Jumamosi, balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa aliwasilisha lalamiko rasmi na kumuandikia barua mkuu wa Baraza la Usalama akitaka kadhia ya Shahidi Fakhrizadeh ichunguzwe.

Bunge la Iran

Wakati huo huo wawakilishi katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), wamesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel wenye kuua watu kiholela ulihusika katika mauaji ya Shahidi Fakhirzadeh. Katika taarifa wabunge wamesema wale ambao katika utawala wa Kizayuni walihusika katika mauaji hayo watalipa gharama ya jinai yao. Wabunge hao wamesema kuuawa shahidi Dkt. Fakhirzadeh, msomi wa nyuklia na sekta ya ulinzi kumewaumiza watu wote wa Iran.

Ijumaa alasiri, Fakhrizadeh aliuawa shahidi baada ya gari lililokuwa limembeba kushambuliwa na magaidi katika mji wa Absard katika eneo la Damavand mkoani Tehran.

Shirika la Utafiti na Ubunifu katika Wizara ya Ulinzi  ya Iran, ambalo lilikuwa likisimamiwa na Shahidi Fakhirzadeh, lilikuwa mstari wa mbele kuunda vifaa vya kupima ugonjwa wa corona. Amesema pia alikuwa akiongoza jitihada za kuunda chanjo ya corona nchini na matokeo ya jitihada hizo yatatangazwa karibuni.