Dec 04, 2020 03:38 UTC
  • Iran yaitaka IAEA iache pasipo na ulazima kueneza taarifa za shughuli zake za nyuklia

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao Vienna ametilia mkazo ulazima wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kuacha, pasipo na ulazima, kueneza taarifa fafanuzi kuhusu shughuli zake za nyuklia.

Kazem Gharib Abadi, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao Vienna ametoa sisitizo hilo katika barua aliyomwandikia Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA akiutaka wakala huo ulaani kwa uwazi kabisa na bila masharti yoyote mauaji ya kigaidi ya Mohsen Fakhrizadeh, mwanasayansi mkubwa wa Iran wa masuala ya nyuklia na ulinzi.

Katika barua hiyo, Kazem Abadi ameashiria ushahidi wa wazi na wa msingi uliopo, unaoonyesha utawala wa Kizayuni ulivyohusika na ulivyo na dhima ya mauaji hayo ya kigaidi na akasisitiza kuwa, IAEA na nchi wanachama wa wakala huo zina masuulia ya msingi kwa Iran ambayo kwa upande mmoja inafanyiwa ukaguzi wa kiwango cha juu kabisa, lakini kwa upande mwingine wanasayansi wake wanaandamwa na vitisho vya kuuliwa au wanauawa huku vituo vyake vya nyuklia vikiandamwa na vitisho au kufanyiwa hujuma za uharibifu.

Kazem Gharib Abadi

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao Vienna amebainisha kwamba, mauaji ya dakta Mohsen Fakhrizadeh ni mwendelezo wa hatua za kigaidi zilizoanza muongo mmoja nyuma kwa kuuliwa wanasayansi kadhaa wa nyuklia wa Iran katika mwaka 2010, 2011 na 2012, hali inayohitaji kupewa uzito na umuhimu maalum na jamii ya kimataifa na mashirika husika ya kimataifa.

Katika barua hiyo, Gharib Kazem Abadi ameeleza pia kwamba, kutunzwa taarifa za siri na wakala wa IAEA kuna umuhimu mkubwa na akasisitiza kuwa, inategemewa kwa msisitizo mkubwa kuuona wakala huo wa atomiki unakomesha katika ripoti zake tabia ya kueneza pasipo na ulazima taarifa fafanuzi kuhusu shughuli za nyuklia za Iran.

Balozi na mwakilishi huyo kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao Vienna amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini ni haki yake ya dhati kujilinda kwa kuchukua hatua zote zinazohitajika ili kujibu mapigo kwa shambulio hilo la kigaidi kulingana na Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kiamataifa.../

Tags