Vifo vya Covid-19 vyaendelea kupungua nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i65042-vifo_vya_covid_19_vyaendelea_kupungua_nchini_iran
Vifo vinavyotokana na Covid-19 vimeendelea kupungua katika siku za karibuni hapa nchini Iran ikiwa ni mafanikio ya kanuni na sheria mbalimbali zilizowekwa na serikali kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya corona.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 06, 2020 08:22 UTC
  • Vifo vya Covid-19 vyaendelea kupungua nchini Iran

Vifo vinavyotokana na Covid-19 vimeendelea kupungua katika siku za karibuni hapa nchini Iran ikiwa ni mafanikio ya kanuni na sheria mbalimbali zilizowekwa na serikali kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya corona.

Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran amesema kuwa, watu wengine zaidi ya elfu 11 wameambukizwa virusi vya corona na wengine 294 wamefariki dunia katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Bi Sima Sadat Lari ameeleza hayo leo wakati alipokuwa akitoa takwimu za karibuni kabisa za maambukizi ya corona hapa nchini na kuongeza kwamba, kwa mujibu wa matokeo ya vipimo rasmi walivyofanyiwa watu wenye maambukizi, katika muda wa masaa 24 yaliyopita wagonjwa wapya 11,561 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 wamegunduliwa humu nchini, ambapo 1,333 miongoni mwao wamelazwa hospitalini na waliobakia wamepatiwa huduma za tiba na kurudi nyumbani.  

Aidha  Dakta Lari  amesema kuwa, idadi ya watu waliogunduliwa kupatwa na ugonjwa wa COVID-19 nchini Iran hadi hivi sasa imefikia 1,040,547 na kuongeza kuwa kufuatia wagonjwa 294 kuaga dunia katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, jumla ya watu waliofariki dunia hadi sasa  hapa nchini kutokana na ugonjwa huo imefikia 50,310.

 

Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran ameongeza kuwa hadi sasa watu 730,798 wamepona maradhi ya Covid-19 hapa nchini au wameruhusiwa kurudi nyumbani. 

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, vifo na maambuzi ya corona nchini Iran yameendelea kupungua katika siku za hivi karibuni kufuatia kanuni na sheria kali zinazotekelezwa na serikali ikishirikiana na Kamati ya Taifa ya Kupambana na Covid-19.