Rais Rouhani: Azma ya Iran ni kustawisha uhusiano wake na Azerbaijan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i65105-rais_rouhani_azma_ya_iran_ni_kustawisha_uhusiano_wake_na_azerbaijan
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uhusiano wa Tehran na Baku ni mzuri na wa kidugu na akaongeza kuwa, azma ya Iran ni kustawisha uhusiano wake na Azerbaijan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 09, 2020 22:01 UTC
  • Rais Rouhani: Azma ya Iran ni kustawisha uhusiano wake na Azerbaijan

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uhusiano wa Tehran na Baku ni mzuri na wa kidugu na akaongeza kuwa, azma ya Iran ni kustawisha uhusiano wake na Azerbaijan.

Rais Rouhani amesema hayo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Jeyhun Bayramov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Azerbaijan ambapo sambamba na kuashiria misimamo bayana na ya wazi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mzozo wa Karabakh  ameeleza kufurahishwa kwake na kuhitimishwa vita katika eneo hilo, kukombolewa maeneo ya Azerbaijan yaliyokuwa yakikaliwa kwa mabavu na kutekelezwa usitishaji vita.

Aidha Dakta Hassan Rouhani amesisitiza juu ya udharura wa kutumiwa mipaka ya Iran na Jamhuri ya Azerbaijan kwa ajili ya kupanua ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara.

Amesema, uwepo na ushiriki wa Iran katika ukarabati wa maeneo yaliyoharibiwa na vita vya Karabakh ni kwa maslahi ya Tehran na Baku.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwa katika mazungumzo na Jeyhun Bayramov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Azerbaijan 09/12/2020-Tehran

 

Rais wa Iran amesema pia kuwa, mazingira yaliyopo ya kutekelezwa makubaliano ya hapo kabla baina ya Iran na Azerbaijan ni hatua ambayo inaweza kupanua zaidi ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali kama za viwanda, elimu, uzalishaji dawa na masuala mengine.

Kwa upande wake, Jeyhun Bayramov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Azerbaijan amepongeza uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu yaIran kwa suala la kulindwa ardhi yote ya Azerbaijan na kueleza kwamba, mipaka ya nchi mbili hizi ni mipka ya kidugu na kirafiki.

Aidha waziri huyo amelaani vikali mauaji ya Mohesn Fakhrizadeh, mwanasayansi bingwa wa nyuklia wa Iran na kusema kuwa, kitendo hicho hakikubaliki hata kidogo.