Amir Abdolahian: Ukoo wa Aal Khalifa umeitia kitanzi demokrasia nchini Bahrain
Msaidizi maalumu wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) katika masuala ya kimataifa amesema kuwa, ukoo wa Aal Khalifa umeitia kitanzi demokrasia nchini Bahrain.
Hossein Amir Abdollahian amesema hayo leo Jumanne kwa mnasaba wa mwaka wa sita wa kukamatwa Sheikh Ali Salman nchini Bahrain na kuongeza kuwa, miaka sita imepita tangu watawala wa Manama wamuweke kizuizini Sheikh Ali Salman, kiongozi wa Jumuiya ya Wifaq ya nchi hiyo.
Amesema, wakati alipotembelea Bahrain, alionana na Sheikh Ali Salman na ilimdhihirikia kipaji chake kikubwa, kwani ni mwanachuoni mwenye muono mpana, mwanamapambano, muumini, mwenye misimamo ya wastani na ni nembo ya mapambano ya kupigania demokrasia nchini mwake.
Ameongeza kuwa, ukoo wa Aal Khalifa umeitia kitanzi demokrasia nchini Bahrain na sasa hivi utawala huo wa kiimla umekuwa mateka wa utawala wa Kizayuni unaotenda jinai kigaidi na kidhulma.
Sheikh Ali Salman alikamtwa na viongozi wa Bahrain tarehe 28 Septemba 2014 kwa madai ya kuifanyia ujasusi Qatar. Baada ya kupachikwa tuhuma hizo na maafisa wa mahakama wa Bahrain, maafisa hao waliamua kumfunga kifungo cha maisha mwanachuoni huyo mwanaharakati, dhulma ambayo ni uvunjaji wa wazi wa haki za binadamu.