Machafuko yanaendelea Darfur Sudan, mwito wa amani watolewa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i65470-machafuko_yanaendelea_darfur_sudan_mwito_wa_amani_watolewa
Licha ya kutolewa miito ya kila namna ya kukomeshwa mapigano ya kikabila huko magharibi mwa Sudan, mapigano bado yanaendelea katika eneo hilo lenye historia ndefu ya machafuko na mapigano.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 29, 2020 08:13 UTC
  • Machafuko yanaendelea Darfur Sudan, mwito wa amani watolewa

Licha ya kutolewa miito ya kila namna ya kukomeshwa mapigano ya kikabila huko magharibi mwa Sudan, mapigano bado yanaendelea katika eneo hilo lenye historia ndefu ya machafuko na mapigano.

Taarifa zinasema kuwa, machafuko hayo yamezushwa na wakimbizi wanaopinga uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kutaka kumalizwa operesheni ya kikosi cha UNAMID katika jimbo la Darfur na kubakisha operesheni ndogo tu ya kisiasa.

Machafuko hayo yametokea mwishoni mwa wiki hii katika mji wa Geneida huko Darfur Kusini baina ya makabila ya Fallata na Masalit. Fujo hizo zimewalazimisha maafisa wa Khartoum ambao wanafanya juhudi za kumaliza uasi na mgogoro katika nchi hiyo iliyotumbukia kwenye mgogoro hasa baada ya maandamano makubwa ya wananchi yaliyoishia kupinduliwa Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo.

Viongozi wa kieneo katika eneo la Darfur Kusini huko Sudan wamesema kuwa, wanajeshi kadhaa wametumwa katika eneo hilo ili kukabiliana na mapigano ya kikabila yaliyoshtadi huko magharibi mwa Sudan.

Wanamgambo wa Darfur

 

Musa Mahdi, Walii wa jimbo la Darfur kusini amesema kuwa, kamati ya usalama ya jimbo hilo imeitisha kikao cha dharura kilichohudhuriwa na makamanda wa jeshi na viongozi wa eneo la Al Qariza; na katika kikao hicho kumesisitizwa kuchukuliwa hatua za kiusalama na kisheria ili kuwasaidia raia na kuwasaka watenda jinai. 

Walii wa eneo la Darfur Kusini ameeleza kuwa, katika kikao hicho kumechukuliwa maamuzi muhimu ikiwemo kutumwa idadi kubwa ya wanajeshi kwa ajili ya kuwakamata watendaji jinai na kukusanya silaha na pia kuunda kamati ya uchunguzi kuhusu matukio yote yaliyojiri katika eneo hilo.