Khatibzadeh amhutubu Pompeo: Dunia imekataa kufanywa mateka wa kuburuzwa na nyinyi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i65497-khatibzadeh_amhutubu_pompeo_dunia_imekataa_kufanywa_mateka_wa_kuburuzwa_na_nyinyi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemhutubu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo kwamba dunia imekataa kufanywa mateka wa kuburuzwa na Marekani.
(last modified 2026-08-17T06:24:47+00:00 )
Dec 31, 2020 00:28 UTC
  • Khatibzadeh amhutubu Pompeo: Dunia imekataa kufanywa mateka wa kuburuzwa na nyinyi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemhutubu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo kwamba dunia imekataa kufanywa mateka wa kuburuzwa na Marekani.

Saeed Khatibzadeh ameyasema hayo sambamba na kuashiria kushindwa na kugonga mwamba kampeni ya mashinikizo ya juu kabisa iliyoendeshwa na Marekani dhidi ya Iran.

Katika jibu alilotoa kwa ujumbe wa twitter ulioandikwa hivi karibuni na Pompeo, aliyedai kwamba Iran ndio chanzo cha kukosekana uthabiti na tishio kwa Marekani na waitifaki wake sambamba na kuzungumzia tena mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya taifa la Iran, Khatibzadeh ameandika katika ukurasa wake wa twitter: baada ya miaka minne ya "kushindwa kwa kiwango cha juu kabisa" Pompeo anatapatapa kwa kuendesha propaganda zisizo na msisimko ili maafa aliyosababisha na kuyashamirisha yaonekane kuwa ni mafanikio kwake.

Saeed Khatibzadeh

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongezea kwa kusema: "habari muhimu: Watu si majuha na dunia imekataa kufanywa mateka wa ubabe wenu. Nendeni zenuni salama usalimini haraka iwezekanavyo!"

Itakumbukwa kuwa baada ya Marekani kujitoa kinyume cha sheria katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA tarehe 8 Mei 2018, ilianzisha kampeni za kiuadui za kila upande ili kuiwekea mbinyo na mashinikizo Iran.

Rais wa nchi hiyo Donald Trump aliahidi kwamba, kwa kujitoa katika JCPOA na kutekeleza sera aliyoipa jina la "Mashinikizo ya Juu Kabisa" ataweza kuilazimisha Iran ikae tena kwenye meza ya mazungumzo ili kufikia kile alichokiita "makubaliano mazuri zaidi" kwa Washington.

Hata hivyo kipindi cha miaka minne ya utawala wa Trump kinamalizika huku akiwa amegonga mwamba katika kufikia lengo lake hilo.../