Brigedia Jenerali Ghaani: Wanafunzi wa Hajj Qasem watawatimua Wamarekani katika eneo hili
Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesisitiza kuwa, kambi ya muqawama inazidi kuwa imara siku baada ya siku na kuongeza kuwa, wanafunzi wa chuo cha shahid Soleimani watawatimua Wamarekani katika eneo hili.
Bigedia Jenerali Esmail Ghaani amesema hayo leo katika sherehe za kwanza za kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu alipouawa shahidi na kidhulma Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kubainisha kwamba, pigo la kwanza alilopata adui baada ya jinai yake hiyo, ni maziko ya kipekee na ya aina yake kabisa aliyopata Kamanda Soleimani, pigo la pili ni kushambuliwa kambi ya Marekani huko Iraq na kudhalilika dola hilo la kibeberu la Marekani kwa kutothubutu kujibu mashambulio hayo.
Brigedia Jenerali Ghaani ameongeza kuwa, kipigo kingine ambacho inabidi akipate adui ni kuishinda haiba bandia ya ubeberu duniani na nne ni kutimuliwa wanajeshi magaidi wa Marekani katika eneo hili.
Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH aidha amewaambia maadui kwa kusisitiza kwamba, kisasi cha damu ya mashahidi kimeanza dhidi yenu na sasa hivi hamna salama wala utulivu hata ndani ya nyumba zenu wenyewe.
Brigedia Jenerali Ghaani pia amesema, watenda jinai wakubwa wa jinai ya kumuua kigaidi Kamanda Soleimani ni rais wa Marekani Donald Trump na waziri wake wa mambo ya nje, Mike Pompeo. Watenda jinai hao wanapaswa kutambua kwamba hawawezi kubakia salama baada ya kuwaua kigaidi na kidhulma mashujaa hao wa eneo la Asia Magharibi.