Kiongozi Muadhamu azungumza na wananchi kwa mnasaba wa Dei 19
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei hivi sasa anaendelea na hotuba yake kwa wananchi kwa mnasaba wa maadhimisho ya mapambano ya Dei 19 ya wananchi wa Qum dhidi ya utawala wa kiimla wa Shah.
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu inarushwa mubashara katika kanali za redio na televisheni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika Intaneti na kwenye mitandao ya kijamii.
Kila mwaka, Kiongozi Muadhamu huhutubia moja kwa moja maelfu ya wananchi wa Qum katika Husainia ya Imam Khomeini MA hapa mjini Tehran. Hata hivyo mwaka huu hotuba hiyo anaendelea kuitoa hivi sasa kwa njia ya televisheni bila ya mahudhurio ya wananchi kama hatua ya kuepusha maambukizo ya kirusi cha corona.
Tarehe 19 Dei 1356 imwaka wa Kiiran wa Hijria Shamsia liyosadifiana na tarehe 9 Januari 1978, walimu na wanafunzi wa chuo cha kidini cha Qum, kusini mwa Tehran walifanya maandamano ya kupinga udhalilishaji uliofanywa na utawala wa kifalme wa Shah dhidi ya Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri y Kiislamu ya Iran. Idadi kubwa ya waandamanaji waliuliwa kidhulma na maafisa usalama wa utawala wa Kipahlavi.
Taarifa kamili kuhusu hotuba hiyo itakujieni katika matangazo yetu yajayo tukijaaliwa.