Zarif akosoa undumakuwili wa Wamagharibi mkabala wa mienendo ya Trump
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i65662-zarif_akosoa_undumakuwili_wa_wamagharibi_mkabala_wa_mienendo_ya_trump
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali undumakuwili wa nchi za Magharibi ambazo hivi sasa zinakosoa mienendo ya kukanyaga utawala wa sheria ya Rais Donald Trump wa Marekani, licha ya kufuata kibubusa sera zake za kibeberu katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Jan 08, 2021 23:12 UTC
  • Muhammad Javad Zarif
    Muhammad Javad Zarif

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali undumakuwili wa nchi za Magharibi ambazo hivi sasa zinakosoa mienendo ya kukanyaga utawala wa sheria ya Rais Donald Trump wa Marekani, licha ya kufuata kibubusa sera zake za kibeberu katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter jana Ijumaa, Muhammad Javad Zarif amewashangaa viongozi wa Magharibi ambao kwa miaka minne walifuata sera za vikwazo za Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, lakini hivi sasa wanajitokeza kulaani ghasia zilizochochewa na mtawala huyo wa Marekani siku ya Jumatano katika Kongresi ya nchi hiyo mjini Washington.

Dakta Zarif amewataka viongozi hao wa Magharibi ambao wanajaribu kutumia sera ya ugaidi wa kiuchumi ya Trump dhidi ya Iran, kuwa na muono wa mbali kwa maslahi ya mataifa yao.

Jumatano iliiyopita,  wafuasi sugu wa Rais Donald Trump walivamia Bunge la Kongresi na kusitisha kwa masaa kadhaa shughuli ya kumuidhinisha rasmi Joe Biden kuwa rais wa 46 wa nchi hiyo.

Wafuasi wa Trump walipovamia majengo ya Kongresi Jumatano

Mbali na uharibifu mkubwa uliosababishwa na wafuasi hao wa Trump, lakini machafuko hayo yalipelekea watu watano akiwemo afisa wa polisi kuuawa.

Ghasia hizo zilitokana na wito wa Trump aliyewataka wafuasi wake kukusanyika mbele ya jengo la Kongresi mjini Washington, ili kuvuruga kikao cha wabunge na maseneta wa nchi hiyo cha kupasisha matokeo ya uchaguzi wa rais na ushindi wa Joe Biden.