Mantiki yenye nguvu ya Iran katika kulinda usalama na kukabiliana na vitisho
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i65684-mantiki_yenye_nguvu_ya_iran_katika_kulinda_usalama_na_kukabiliana_na_vitisho
Miongoni mwa sehemu muhimu ya siasa za kiulinzi za Iran ni kuimarisha uwezo wa kujihami wa makombora ambao una umuhimu wa kistratejia na kimkakati katika masuala yanayohusiana na kuimaisha uwezo wa kijeshi na kukabiliana na vitisho vya adui.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Jan 09, 2021 22:57 UTC
  • Mantiki yenye nguvu ya Iran katika kulinda usalama na kukabiliana na vitisho

Miongoni mwa sehemu muhimu ya siasa za kiulinzi za Iran ni kuimarisha uwezo wa kujihami wa makombora ambao una umuhimu wa kistratejia na kimkakati katika masuala yanayohusiana na kuimaisha uwezo wa kijeshi na kukabiliana na vitisho vya adui.

Katika mkondo huo, jana Ijumaa kulizinduiwa moja ya vituo vya makombora vya vikosi vya majini ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) katika pwani ya Ghuba ya Uajemi katika sherehe iliyohudhuriwa na Kamanda Mkuu wa Jeshi la Sepah. 

Meja Jenerali Hussein Salami amesema katika hafla ya uzinduzi wa kituo hicho kwamba: Mantiki yetu katika kulinda ardhi yote ya Iran ni kujitawala nchi na kulinda mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu. Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Ili kuzuia kutwishwa matakwa ya madola ya kibeberu na njama zao hakuna njia nyingine ghairi ya kuimarisha uwezo wa kiulinzi wa kukabiliana na mashambulizi na uvamizi wa aina yoyote. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina mzaha na yoyote katika masuala yanayohusiana na usalama wa nchi hii na ni kwa msingi huo ndio maana imezidisha uwezo wake wa kijeshi wa kukabiliana na vitisho vya adui. 

Meja Jenerali Hussein Salami

Ayatullah Khamenei Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza mara kadhaa katika hotuba zake kuwa: Lengo la siasa za kuimarisha nguvu za kujilinda za utawala wa Kiislamu hapa nchini ni kuzuia hata dhana na nia ya madola ya kibeberu ya kutaka kuishambulia Iran. 

Katika sehemu moja ya hotuba yake Ijumaa iliyopita pia ambayo ilirushwa mubashara na televisheni ya Iran kwa mnasaba wa kumbukumbu ya maadhimisho ya mapambano ya wananchi wa mji mtakatifu wa Qum tarehe 19 mwezi Dei mwaka 1356, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikumbusha tajiriba chungu ya kushindwa nchi kukabiliana na mashambulizi ya anga ya Saddam Hussein na kueleza kuwa: Wakati huo Iran haikuwa na uwezo wa kukabiliana na kujilinda na makombora yaliyokuwa yakivurumishwa dhidi ya Tehran na katika miji mingine ya nchi hii, na Jamhuri ya Kislamu ya Iran haikuwa na haki ya kuiacha nchi katika hali kama hiyo bila kuchukua hatua.  

Kiongozi Muadhamu aidha ametoa mifano ya nguvu za kiulinzi za Iran hii leo kama kutunguliwa ndege isiyo na rubani ya Marekani katika anga ya Iran na jinsi Iran ilivyosambaratisha kambi ya kijeshi ya nchi hiyo ya Ain al Asad huko Iraq na kueleza kuwa: Kwa kutilia maanani ukweli wote, adui analazimika kutilia maanani nguvu na uwezo wa kiulinzi wa Iran katika mahesabu na maamuzi yake.  

Ayatullah Khamenei

Marekani inayotenda jinai mwaka mmoja uliopita ilidhihirisha chuki na uhasama mkubwa dhidi ya Iran na tarehe tatu mwezi Januari mwaka 2020 ikatekeleza hujuma ya kigaidi kwa kuwauwa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (Sepah) na wenzake kadhaa waliokuwa wakifuatana naye huko Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo. Mauaji hayo yalitekelezwa kwa   amri ya moja kwa moja ya Donald Trump.

Jeshi la Sepah tarehe 8 mwezi huo huo wa Januari mwaka jana lilijibu vikali jinai hiyo ya Marekani kwa kuvurumisha makombora 13 katika kambi ya kijeshi ya Marekani ya Ain al Asad katika mkoa wa al Anbar magharibi mwa Iraq. Jibu hilo kali lilionyesha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo mkubwa kwa upande nguvu za kiulinzi na kujibu mashambulizi ya adui. 

Katika taarifa yao iliyotolewa mwezi Agosti mwaka jana kwa mnsaba wa maadhimisho ya Siku ya Viwanda vya Zana za Ulinzi, wawakilishi wa Bunge la Iran waliashiria udharura wa kuwa tayari kwa ajili ya kulinda nchi na kutilia mkazo umuhimu wa kustawishwa zaidi uwezo wa makombora na zana za kujihami za Jamhuri ya Kiislamu. 

Kwa sasa uwezo wa kujihami na kukabiliana na hujuma na vitisho vya adui wa Iran uko katika kiwango cha juu. Katika upande wa maendeleo ya zana za ulinzi wa anga, kwa sasa Iran inashika nafasi ya tano kati ya nchi zilizopiga hatua kubwa zaidi katika utengenezaji wa ndege zisizo na rubani na inahesabiwa kuwa ya pili katika utengnezaji wa drone zisizoonekana kwa rada. 

Ndege zisizo na rubani za Iran

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Shihab Shaabani anasema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbali na kuwa na tajiriba na uzoefu wa miaka nane ya vita, inahesabiwa kuwa nguvu ya tano kubwa zaidi duniani kwa kuwa na uwezo wa makombora. Kwa msingi huo ni wazi kuwa, adui yeyote anayekusudia kuishambulia Iran analazimika kwanza kupima kiwango cha faida na hasara za shambulizi kama hilo.."