Khatibzadeh: Iran haijafanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hakujafanyika mazungumzo ya moja kwa moja baina ya taifa hili na Marekani na kwamba, maelezo yanayobainishwa na kuonyesha kama kumekuweko na mazungumzo ya moja kwa moja baina ya Tehran na Washington hayana ukweli wowote.
Saeed Khatibzadeh amesema kuwa, Iran imepokea baadhi ya jumbe kutoka kwa serikali mpya ya Marekani kupitia ubalozi wa Uswisi hapa mjini Tehran ambao ndio unaolinda maslahi ya Marekani na baadhi ya wizara za mashauri ya kigeni za mataifa mengine, zinaoeleza utayari wa Washington wa kubadilishana wafungwa.
Kuhusiana na suuala la wafungwa, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran imekuwa ikifuatilia kuachiliwa huru wafungwa Wairani huko nchini Marekani ambao kimsingi wamekamatwa na kushikiliwa pasi na kufanya uhalifu au kosa.
Aidha Khatibazdeh ameongeza kuwa, wafungwa hao wa Kiirani wanaishi katika mazingira mabayana mahala wanaposhikiliwa, na kwamba, serikali inalipa kipaumbele suala la kufuatilia na kuhakikisha wafungwa hao wanaachiliwa huru.
Jake Sullivan, mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani alisema jana kuwa, Washington imeanza kufanya mawasiliano na Tehran kuhusiana na wafungwa wa Kimarekani walioko katika jela za Iran na kwamba, itafuatilia suala hilo kuhakikisha kwamba, wafungwa hao wanaachiliwa huru na kurejea nyumbani.
Aidha alisisitiza kuwa, hilo ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na serikali mpya ya Marekkani chini ya uongozi wa Rais Joe Biden.