Iran: Hatuoni mabadiliko yoyote katika vitendo vya Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran haioni mabadiliko yoyote katika vitendo vya Marekani licha ya rais mpya kuingia madarakani nchini humo
Shirika la habari la IRIB limemnukuu Dk Mohammad Javad Zarif akisema hayo katika ujumbe wake wa Twitter wa jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, Marekani inakiri kwamba hata baada ya nchi hiyo kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Iran imeendelea kuheshimu makubaliano hayo ya kimataifa licha ya kuchukua hatua za kupunguza ahadi zake.
Zarif amesema, vitendo vya Marekani ambavyo ndivyo vilivyoilazimisha Iran kupunguza ahadi zake ndani ya JCPOA, havijabadilika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesisitiza kuwa, nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani nazo ni wakosa kwani katika kipindi chote hiki cha miaka mitatu iliyopita hazijafanya biashara yoyote na Iran.
Amesema, nchi hizo tatu za Ulaya pamoja na Marekani zinapaswa kutekeleza ahadi zao kwanza na sio kuitaka Tehran iache hatua zake ambazo isingelizichukua kama si vitendo vya nchi hizo za Magharibi.
Baada ya Marekani kujitoa bila ya sababu katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA hapo tarehe 8 Mei 2018 na kuirejeshea Tehran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa mapatano hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tena baada ya kuvumilia mwaka mzima, iliamua nayo kuchukua hatua za kukabiliana na uvunjaji ahadi wa Marekani na nchi tatu za Ulaya, kupitia kupunguza utekelezaji wa ahadi zake ndani ya mapatano hayo awamu kwa awamu.