Tehran: Vikwazo vya Marekani vimekiuka haki za raia wa Iran
Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa amesema kuwa vikwazo vya upande mmoja, haramu na vya kidhalimu vya Marekani vimekiuka haki za taifa la Iran na nchi hiyo haina haki ya kuzungumzia au kuwa na wasiwasi kuhusu haki za binadamu nchini Iran.
Sayyid Mohammad Sadati Nejad ambaye alikuwa akihutubia kikao hicho mjini Geneva, amesema kuwa, serikali ya sasa ya Marekani inaendeleza siasa zilizofeli za mashinikizo ya kiwango cha juu za utawala wa Donald Trump dhidi ya taifa la Iran, na siasa hizo ni ugaidi wa kiuchumi dhidi ya taifa zima.
Ameongeza kuwa, Marekani pia inapaswa kuwajibishwa kwa sababu ya kuwatia nguvuni raia wa Iran waliokuwa wakifanya jitihada za kukwepa vikwazo haramu vya serikali ya Washington.
Sadati Nejad amesema kuwa, taifa la Iran kamwe halitasahau ugaidi wa Marekani ikiwa ni pamoja na mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu akiwa katika safari rasmi ya kikazi nchini Iraq.
Itakumbukwa kuwa tarehe 8 Mei mwaka 2018 aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump alikanyaga sheria za kimataifa na kuiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA kisha akaanzisha tena vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.