Zoezi la kuwasajili wanaotaka kugombea urais Iran laingia siku ya nne
Zoezi la kuwasajili wale wanaotaka kuwania urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limeingia siku ya nne leo.
Kwa mujibu wa taarifa, zoezi hilo limeanza leo saa mbili asubuhi katika Makao Makuu ya Uchaguzi ambayo yako katika Wizara ya Mambo ya Ndani mjini Tehran.
Msemaji wa Makao Makuu ya Uchaguzi katika Wizara ya Mambo ya Ndani Sayyid Ismail Mousavi alisema jana Alhamisi watu 81 walijiandikisha wakitaka wawe wagombe wa kiti cha urais. Amesema katika siku tatu za kwanza za kujiandikisha jumla ya watu 211 wamesajili majina yao wakitaka waidhinishwe kuwa wagombea wa urais.
Baada ya kumalizika uandikishaji huo unaofanyika kwa muda wa siku tano, majina ya wagombea wenye azma ya kuwania urais katika uchaguzi wa mwezi ujao yatakabidhiwa Baraza la Kulinda Katiba.

Baraza hilo lenye wanachama 12 litatathmini na kuyapiga msasa majina hayo, na kuwapasisha watakaokuwa wamekidhi vigezo na masharti ya kisheria kugombea urais hapa nchini.
Miongoni mwa watu mashuhuri waliojiandikisha kugombea urais ni rais wa zamani Mahmoud Ahmadinejad, na mawaziri wake wa zamani wakiwemo waziri wa zamani wa mafuta Rostam Ghasemi, waziri wa zamani wa michezo Mohammad Abbasi na waziri wa zamani wa kilimo Sadegh Khalilian.
Uchaguzi wa rais wa awamu ya 13 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatazamiwa kufanyika 18 Juni.