Kiongozi Muadhamu atoa onyo kali kuhusu midahalo ya wagombea urais Iran
Ukurasa wa Twitter wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kislamu umetuma ujumbe wa indhari kuhusu kuwavunjia wengine heshima katika midahalo ya wagombea wa urais wa Iran huku akitoa onyo kali kuhusu sualaa hilo.
Katika radiamali baada ya mdahalo wa kwanza wa wagombea urais wa Iran uliofanyika jana alasiri, ukurasa wa Instagram wa Kiongozi Muadhamu pia umenukulu hotuba yake na kuandika: "Kila wakati ambapo katika midahalo ya televisheni wagombea wanatumia mbinu ya kuvunjiana heshima, kutuhumu na kuharibia jina upande wa pili na kuwatisha wananchi kuhusu mshindani, hilo huwa ni kwa hasara ya nchi."
Mdahalo wa kwanza baina ya wagombea urais nchini Iran uliofanyika kupitia televisheni ya taifa uliendelea kwa muda wa masaa matatu.
Kila mgombea anapewa muda wa kutosha wa kueleza sera na mipango yake iwapo atachaguliwa na wananchi, kupitia redio na televisheni ya taifa ya kujibu maswali ya wananchi, wataalamu na waandishi wa habari.
Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) linatayarisha mdahalo huo ambao utawashirikisha wagombea wote saba wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Kiislamu.
Wagombea urais katika uchaguzi wa mwaka huu nchini Iran ni Saeed Jalili, Mohsen Rezaee Mirgha'ed, Sayyid Ebrahim Raisi, Alireza Zakani, Sayyid Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi, Mohsen Mehralizadeh na Abdolnaser Hemmati.
Rais wa sasa Hassan Rouhani anakamilisha muhula wake wa pili mfululizo na hivyo haruhusiwi kugombea awamu hii kisheria.
Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi nchini Iran, kampeni za uchaguzi za wagombea wa urais zilianza rasmi tarehe 25 Mei ambapo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran ilitangazwa majina ya wagombea. Kampeni hizo zinaendelea hadi masaa 24 kabla ya kuanza zoezi la kupiga kura.
Wagombea wote nchini Iran wanapewa haki sawa kwa kuhesabiwa mpaka sekunde za kufanya kampeni katika Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, bila ya kupunguziwa au kuongezewa hata sekunde moja.
Uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uchaguzi wa 6 wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe 18 mwezi ujao wa Juni, 2021.