Iran yalaani shambulio la kigaidi la nchini Burkina Faso
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani shambulizi ya kigaidi lililofanywa na magenge yenye silaha nchini Burkina Faso.
Saeed Khatibzadeh alisema hayo jana Jumapili na sambamba na kulaani shambulio hilo la kigaidi amesema kuwa, Iran iko tayari kutoa msaada wowote unaohitajika na kutumia uzoefu wake katika kupambana na mgaidi kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Vile vile amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesikitishwa sana na kuuliwa bila ya hatia watu wa kawaida huko Burkina Faso, nchi ambayo inashuhudia vitendo vingi vya kigaidi kutokana na kupakana na nchi kama Mali na Niger.
Serikali ya Burkina Faso imetangaza kuwa, watu wenye silaha walikivamia kijiji kimoja cha kaskazini mwa nchi hiyo nyakati za usiku na kuwaua kwa umati watu 100.
Katika miaka ya hivi karibuni, Burkina Faso imekuwa ikishuhudia mashambulizi mengi ya kigaidi. Mashambulizi hayo yalianzia kaskazini mwa nchi hiyo na baadaye kuenea katika maeneo ya mashariki na katikati mwa nchi.
Mashambulio hayo yaliyoanza mwaka 2015 yameshapelekea mamia ya watu kuuawa na yamesababisha hasara kubwa kwa mali za umma.
Mashambulio mengi ya kigaidi yanatokea katika maeneo ya mpakani mwa Burkina Faso na nchi za Mali na Niger ambazo nazo zinashuhudia mashambulio mengi makubwa na ya mara kwa mara ya magenge ya kigaidi.