Jibu la Iran kwa matamshi na ripoti za Mkurugenzi Mkuu wa IAEA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i71048-jibu_la_iran_kwa_matamshi_na_ripoti_za_mkurugenzi_mkuu_wa_iaea
Ripoti ya hivi karibuni ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuhusu Iran inatokana na muelekeo wa upande mmoja wa wakala huo ambao unapuza ushirikiano wa kiufundi na muelekeo kama huo unaweza kuwa kizingiti katika ushirikiano wa pande mbili katika siku za usoni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 08, 2021 21:56 UTC
  • Jibu la Iran kwa matamshi na ripoti za Mkurugenzi Mkuu wa IAEA

Ripoti ya hivi karibuni ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuhusu Iran inatokana na muelekeo wa upande mmoja wa wakala huo ambao unapuza ushirikiano wa kiufundi na muelekeo kama huo unaweza kuwa kizingiti katika ushirikiano wa pande mbili katika siku za usoni.

Hiyo ni sehemu ya kauli ya Kazem Gharibabadi, Balozi wa Iran katika mashirika ya kimataifa yaliyoko Vienna, Austria katika kujibu ripoti ya  Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Raphael Grossi.

Jumatatu wakati wa kuanza kikao cha Bodi ya Magavana wa  IAEA, Grossi alidai kuwa, uwezo wa wakala huo wa kuweza kufuatilia 'malengo ya amani' katika miradi ya nyuklia ya Iran unaweza kuathiriwa vibaya na kile alichokitaja kuwa 'ukosefu wa maendeleo' katika kujibu masuali ya wakala huo kuhusu shughuli za nyuklia za taifa hili. Alitoa madai pia kuhusu kile alichokitaja kuwa eti ni shughuli za nyuklia za Iran ambazo hazijatangazwa.

Taarifa ya Grossi haijazingatia uhalisia wa mambo na inalenga kufanikisha malengo ya Marekani. Sambamba na kikao cha Bodi ya Magavana wa IAEA mjini Vienna, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony  Blinken akizungumza katika Kamati ya Sera za Kigeni ya Baraza la Wawakilishi Marekani, ambapo bila kutaja kuwa Marekani imekiuka ahadi zake katika mapatano ya JCPOA, alidai kuwa bado haijulikani iwapo Iran inataka kurejea katika mapatano ya JCPOA au la.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amemjibu Blinken kupitia ukurasa wa Twitter na kusema: "Hadi sasa haijulikani iwapo serikali ya Marekani iko tayari kuweka kando siasa za rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump na waziri wa zamani wa mashauri ya kigeni wa nchi hiyo, Mike Pompeo au la. Hadi sasa haijulikani kama Rais wa Marekani na Antony Blinken wako tayari kutupilia mbali sera za mashinikizo ya kiwango cha juu za Trump na Pompeo na kukoma kutumia ugaidi wa kiuchumi kama wenzo wa mashinikizo au la. Iran inashikamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA; soma kifungu nambari 36 za JCPOA. Bado kuna fursa ya kufanya mabadiliko."  

Kwa mujibu wa vifungu vya 26 na 36 vya JCPOA, iwapo upande mmoja haufungamani na mapatano, upande wa pili katika mapatano hayo ya kimataifa, yaani Iran, ina haki ya kusitisha utekelezaji wa ahadi zake katika mapatano hayo. 

Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran mnamo Mei 8 2019, yaani mwaka moja baada ya Marekani kuchukua hatua ya upande mmoja kujiondoa JCPOA, lilitangaza kuwa, Iran itaanza kupunguza hatua kwa hatua utekelelzaji wa ahadi zake katika JCPOA kwa mujibu wa vifungu nambari 26 na 36 vya JCPOA. Lengo la hatua hiyo ya Iran limetajwa kuwa ni kuleta mlingano baina ya  utekelezaji wa ahadi zake  na haki zake. Aidha katika utekelezaji wa sheria ya "Hatua ya Kistratijia ya Kuondoa Vikwazo na Kulinda Haki za Iran" ilipitishwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran). Sheria hiyo ilisitisha hatua za kujitolea za Iran katika  JCPOA ikiwa ni pamoja na Protokali Ziada ya masuala ya nyuklia.

Pamoja na hayo,  Iran, kwa mujibu wa mapatano yake na na IAEA, ilitangaza kuwa, iwapo vikwazo vya Marekani vitaondolewa kikamilifu katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Mwezi Februari mwaka huu, basi  itaipa IAEA data zote zilizonaswa na kamera katika vituo vyake vya nyuklia na iwapo vikwazo havitaondolewa Iran itafuta kabisa taarifa zote zilizonaswa na kamera hizo.

Muda uliokuwa umeainishwa katika mapatano hayo ulimalizika mwezi uliopita na kwa kuzingatia kuwa mazungumzo ya nyuklia ya Iran yangalia yanaendelea huko Vienna, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliafiki kusitisha utekelezwaji wa mapatano hayo hadi 24 Juni. Mwakilishi wa Iran mjini Vienna amezishauri nchi zinazofanya mazungumzo na Iran Vienna ambazo ni Russia, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani pamoja na mwakilishi wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, kutumia fursa ambayo imetolewa kutokana na nia njema ya Iran. Amezitaka nchi hiyo kuhakikisha kuwa vikwazo vinaondolewa kikamilifu. Kwa msingi hiyo ripoti mpya ya Grossi ni kinyume cha mchakato wa mazungumzo ya Vienna na ni wazi kuwa inalenga kuishinikiza Iran sambamba na mazungumzo hayo.