Zarif: Kuna wajibu wa kuodolewa vikwazo vyote dhidi ya Yemen, haraka iwezekanavyo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekutana na mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen na kusema kuwa, kuna wajibu na udharura wa kuondolewa haraka vikwazo walivyowekewa wananchi wa Yemen.
Dk Mohammad Javad Zarif alisema hayo jana Jumanne wakati alipoonana na Martin Griffiths, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa Yemen na kusema kuwa, kadiri vikwazo na mzingiro dhidi ya Yemen unavyoendelea, ndivyo wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu wanavyozidi kuumia.
Vile vile amebainisha siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilizosimama juu ya msingi wa kupinga vita na kusema kuwa, Tehran inaamini kwamba mgogoro wa Yemen hauwezi kutatuliwa kijeshi, njia pekee ya kuutatua mgogoro huo ni mazungumzo ya kisiasa na njia za kiusalama. Amekumbusha kuwa, kwa zaidi ya miaka 6 sasa wananchi wa Yemen wamo kwenye janga kubwa la kibinadamu.
Kwa upande wake Martin Griffiths amesema katika mazungumzo yake hayo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba, mazungumzo yao yalikuwa chanya na pande mbili zimetilia mkazo udharura wa kutatuliwa haraka mgogoro wa Yemen.
Pande hizo mbili zimejadiliana kwa kina pande mbalimbali za mgogoro wa Yemen na kubadilishana mawazo juu ya njia bora zaidi za kuleta amani na utulivu katika nchi hiyo.
Huku ikiungwa mkono kikamilifu na Marekani, utawala wa Kizayuni, Imarati, Sudan na nchi nyingine kadhaa, Saudi Arabia ilianzisha uvamizi na mashambulizi ya pande zote dhidi ya nchi maskini ya Yemen mwezi Mei mwaka 2015 na kisha kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, angani na nchi kavu hadi leo hii.