Iran yaitaka IAEA kuacha sera za upendeleo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i71128-iran_yaitaka_iaea_kuacha_sera_za_upendeleo
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika jumuiya za kimataifa huko Vienna nchini Austria ameutaka Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuacha sera za upendeleo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 10, 2021 21:44 UTC
  • Iran yaitaka IAEA kuacha sera za upendeleo

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika jumuiya za kimataifa huko Vienna nchini Austria ameutaka Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuacha sera za upendeleo.

Kazem Gharibabadi amekiambia kikao cha Baraza la Magavana la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kwamba kimya cha wakala huo mbele ya vitisho vya utawala wa Kizayuni wa Israel vya kutumia silaha za nyuklia dhidi ya nchi mbalimbali na vitendo vya kigaidi na uharibifu vya utawala huo dhidi ya taasisi za nyuklia nchini Iran, kimezusha maswali mengi kuhusu hadhi na madai ya kutopendela upande wowote ya shirika hilo.

Balozi Gharibabadi ameongeza kuwa, katika miaka ya nyuma maudhui ya miradi ya nyuklia ya Iran ilikuwa ikijadiliwa katika wakala wa IAEA kwa kutegemea madai yasiyo na msingi japokuwa hadi sasa hakujapatikana hata waraka mmoja unaoonyesha kuwa miradi hiyo imekengeukka sheria. Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuheshimu majukumu yake katika wakala huo.

Makao makuu ya IAEA

Vilevile amesema hujuma ya kigaidi ya tarehe 11 Aprili mwaka huu wa 2021 dhidi ya taasisi ya nyuklia ya Iran ingeweza kusababisha maafa ya kjibinadamu na katika mazingira. Ametoa wito wa kuchukuliwa hatua na kuwajibishwa wahusika wa jinai hiyo.

Mwakilishi wa Iran katika jumuiya za kimataifa mjini Vienna amesema vyombo vya habari vya Israel na nchi za Magharibi vimefichua kwamba Israel ilihusika na hujuma hiyo ya kigaidi.