Balozi: Kenya na Iran kuimarisha uhusiano wao katika uga wa TEHAMA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i71228-balozi_kenya_na_iran_kuimarisha_uhusiano_wao_katika_uga_wa_tehama
Balozi wa Iran nchini Kenya amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuzipa uzoefu wake kampuni za kitaalamu za Kenya, na kuunda jukwaa la kubadilishana mawazo juu ya masuala ya teknolojia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 13, 2021 21:55 UTC
  • Balozi: Kenya na Iran kuimarisha uhusiano wao katika uga wa TEHAMA

Balozi wa Iran nchini Kenya amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuzipa uzoefu wake kampuni za kitaalamu za Kenya, na kuunda jukwaa la kubadilishana mawazo juu ya masuala ya teknolojia.

Jafar Barmaki alisema hayo jana Jumapili katika mkutano baina ya wafanyabiashara na wawekezaji wa Iran na Kenya uliofanyika kwa njia ya intaneti na kusisitiza kuwa, kuimarika uhusiano wa Tehran na Nairobi katika uga wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutatoa mchango mkubwa katika kuimarika zaidi uhusiano wa kibiashara wa pande mbili.

Balozi Barmaki ameuambia mkutano huo kuwa: Iran ina mipango ya kuarifisha fursa za uwekezaji kwa wafanyabiashara wa Kenya, na kwamba katika uwanja huo, Eneo la Uzalishaji wa Uchumi wa Iran (Iranian Economic Processing Area) kama uga wa kuimarisha ushirikiano wa pande mbili limekamilika, na karibuni hivi litaamilishwa.

Mwakilishi huyo wa Iran nchini Kenya ameshiria uzinduzi uliofanyika mapema mwaka huu wa Kituo cha Ubunifu na Teknolojia cha Iran (IHIT) katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi na kusisitiza kuwa, kituo hicho kitaimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya Iran na Kenya, bali hata na nchi nyingine za kanda ya Afrika Mashariki.

Itakumbukwa kuwa, Januari mwaka huu 2021, Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia, Dakta Sorena Sattari akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo jijini Nairobi, alisema Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono kikamilifu ushirikiano baina ya Nairobi na Tehran katika uga wa teknolojia.

Sattari akizungumza katika uzinduzi wa IHIT mjin Nairobi Jan 2021

Aliashiria mafanikio ya Iran katika uzalishaji wa vifaa na suhula za matibabu katika kipindi hiki cha janga la corona na kueleza kuwa, ili kuweza kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19, kampuni za kitaalamu za Iran zimefanikiwa kuzalisha vifaa mbalimbali vya tiba kama mashine za hewa ya oksijeni zinazohitajika na waliokumbwa na ugonjwa wa Covid-19, vipimajoto vya kidijitali, mashine za kupiga picha mwili wa mwandamu za CT Scan n.k.

Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) wa Kenya, Joseph Mucheru na Rais wa Jumuiya ya Biashara ya Kenya ni mingoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria uzinduzi huo wa Kituo cha Ubunifu na Teknolojia cha Iran (IHIT) katika mtaa wa Kilimani jijini Nairobi.